Robertinho aipigia hesabu upya Wydad

LICHA ya kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Wydad Casablanca, Kocha Mkuu wa Simba, Roberto Oliveira, amesema kuwa bado kazi haijaisha wanarudi kwenye uwanja wa mazoezi kujiandaa na dakika 90 zijazo nchini Morocco.

Ushindi huo unaifanya Simba kutanguliza mguu mmoja  nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ikihitaji sare  ama ushindi wa  aina yoyote ili kuweka rekodi  ya kutinga hatua hiyo kwa mara ya kwanza.

Akizungumza juzi Kocha Roberto Oliviera ‘Robertinho’ alisema kuwa anawapongeza wachezaji wake kwa kufuata maelekezo aliyowapa na kufanikiwa kupata ushindi wa bao moja ambao haukuwa rahisi kutokana na aina ya wapinzani waliokutana nao.

“Nawapongeza wachezaji wangu kwa kiwango safi, haikuwa mechi rahisi tumecheza na timu kubwa lakini tumefanya vizuri lakini pia nawapongeza wapinzani wetu Wydad kwa kucheza vizuri kwenye kuzuia hasa wakijua wapo ugenini,”.

“Timu yetu inazidi kuimarika kila siku, tuna wachezaji bora, kwa sasa kila timu inayopangwa nasi inapaswa kutuheshimu kama ambavyo sisi tunawaheshimu,” alisema Robertinho.

Akizungumzia mchezo wa marudiano utakaopigwa wikiendi ijayo nchini Morocco, Robertinho alisema kuwa kila mchezo una mipango yake na mbinu zake anarudi kwenye uwanja wa mazoezi kujiandaa na mchezo huo ambao utatoa taswira ya nani atasonga hatua inayofuata.

Kocha wa Wydad, Leo (juzi )  Juan Carlos Garrido, alisema wamecheza mchezo wa kwanza wa raundi hii wamepambana lakini hajafurahishwa na matokeo kulikuwa na baadhi ya mambo hayakuenda anavyotaka wanaenda kukaa chini na kufanya tathimini na kujiandaa na mchezo ujao ili washinde na kufuzu hatua inayofuata.

“Tulitengeneza nafasi tatu hadi nne za kufunga lakini tukashindwa kufanya hivyo na hiyo ndio tofauti hatua hii ina michezo miwili tumecheza nusu ya kwanza tunaenda kucheza nusu nyingine kama timu matokeo haya yametutia hamasa lengo letu ni kushinda na kwenda hatua inayofuata,” alisema Garrido.

Habari Zifananazo

Back to top button