MKURUGENZI Mtendaji wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KIA), Christine Mwakatobe amesema jumla ya watalii 527 wamerejea Israel baada ya kutembelea vivutio mbalimbali nchini katika Sikukuu ya Pasaka.
Akizungumza jana katika Kiwanja cha KIA mkoani Kilimanjaro, Mwakatobe alisema watalii hao walikuja nchini kuadhimisha Sikukuu ya Pasaka kwa kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii zikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Tarangire na Ngorongoro.
“Mtakumbuka kuwa siku kadhaa zilizopita zaidi ya watalii 240 kutoka Israel walichagua kusherehekea Sikukuu ya Pasaka kwa kutembelea vivutio vya utalii nchini, wamefanya hivyo na leo (jana) watalii 527 wameondoka kurejea nchini mwao,” alisema Mwakatobe.
Alisema watalii hao ni matokeo ya juhudi kubwa zinazofanywa na mamlaka mbalimbali nchini za kutangaza vivutio vilivyoko nchini ikiwemo filamu ya The Royal Tour iliyozinduliwa mapema mwaka jana na kuoneshwa katika kumbi mbalimbali za filamu duniani.
Ofisa Utalii wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Kanda ya Kaskazini, Esther Solomon alisema watalii hao ni matokeo ya jitihada zinazofanywa kutangaza vivutio vya utalii nchini na kuwa idadi ya watalii wanaoingia nchini inaongezeka siku hadi siku.
Wakizungumza kabla ya kuondoka kurejea Israel wakiwa kiwanjani hapo, baadhi ya watalii walisema wanafurahi kutembelea vivutio hivyo na kusema Tanzania ni miongoni mwa maeneo bora zaidi yenye vivutio vya utalii duniani.
Mwongoza watalii kutoka Israel, Shlomo Carmel alisema safari yao ilikuwa nzuri na yenye msisimko kwani Tanzania ni eneo bora la utalii.
“Tanzania ni eneo bora na zuri zaidi kwa utalii, tumefurahi sana na hakuna hata mmoja wetu amelalamikia kitu chochote, hii ndiyo ‘Unforgotten Tanzania’ tuko pamoja,” alisema Carmel.
Alisema kundi alilokuja nalo linaondoka lakini limeahidi kuwa kipindi cha kiangazi watarejea tena Tanzania kutembelea vivutio hivyo na vingine pamoja na kupumzika.
Mapema wiki iliyopita, TTB ilitoa taarifa ikielezea ujio wa wageni hao kutoka Israel ambao walisema wamefika kwa ajili ya kusherehekea Sikukuu ya Pasaka kwa kutembelea vivutio vya utalii nchini.
Mbali ya kutembelea vivutio hivyo maeneo ya Kaskazini mwa nchi, pia walitembelea fukwe za Zanzibar na maeneo ya urithi.
TTB ilizindua kampeni ya kuongeza idadi ya watalii wanaoitembelea Tanzania kutoka Israel, huku pia Watanzania wakisafiri kwenda nchini humo kwa ajili ya hija za kidini.
Historia inaeleza kuwa taifa la Israel ni moja ya nchi Takatifu ya Kikristo na makundi makubwa ya wageni kutoka Afrika na mataifa mengine duniani hutembelea maeneo ya nchi hiyo ya kihistoria ya kidini, mfano katika Mji wa Yerusalemu, Nazareti na Bethlehemu, Bahari ya Galilaya na maji ya uponyaji na matope ya Bahari ya Chumvi.
Mahujaji wa Kikristo wa Kiafrika hutembelea Israel kati ya Machi na Aprili kila mwaka ili kutoa heshima katika maeneo matakatifu Israel na Yordani.
Tanzania ni miongoni mwa nchi za Kiafrika zinazotangaza utalii wao nchini Israel ili kuvutia wageni wa Israel.
Kampuni kadhaa kutoka Mji wa Tel Aviv, zinatangaza vivutio vya utalii Afrika nchini Israel ambao umevutia maelfu ya watalii wanaokuja kwa wingi sasa kuvitembelea.