KAMANDA wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Wilbroad Mutafungwa amewapongeza maafisa, wakaguzi na askari wa vyeo mbalimbali wa Mkoa wa Mwanza kwa kazi nzuri ya kudhibiti na kupunguza uhalifu kwa mwaka 2023 na kutoa mwelekeo wa mwaka 2024.
RPC Mutafungwa ametoa pongezi hizo katika kikao cha baraza na askari hao lililolenga kupima tathmini ya utekelezaji wa mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai kwa Jeshi la Polisi yaliyoibuliwa na tume hiyo iliyoongozwa na Jaji Mstaafu Othman Chande mwaka 2023.
Pongezi hizo zimetolewa Januari 8, 2024 katika uwanja wa polisi Mabatini kwa askari wote hususan Kikosi cha Usalama Barabarani ambapo amesema kuwa malalamiko katika kikosi hicho yamepungua ukilinganisha na miaka ya nyuma.
“Mimi kama kiongozi wenu nichukua nafasi hii kuwapongeza kwa dhati kwa kazi nzuri ya kuhakikisha Mkoa wetu unakuwa salama, sio kwamba uhalifu umeisha, ninawapongeza kwa sababu zipo jitihada kubwa mnazofanya za kumaliza uhalifu zikiongozwa na Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa.” Alisema Kamanda Mutafungwa.
Kuhusu vipaumbele vya kudhibiti uhalifu 2024, Kamanda Mutafungwa ametoa mwelekeo wa utekelezaji wa kazi za Polisi na kuahidi kuwa askari Polisi atakayejihusisha na vitendo vya rushwa, kubambikiza watu kesi, kufanya kazi kwa mazoea na kutoa lugha chafu kwa wateja hatofumbiwa macho.
Aidha kwa upande wake Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Mwanza Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Yesaya Sudy ameahidi kwenda kuyatekeleza yale yote yaliyoelekezwa na kufanya upelelezi wa haraka kwa askari yeyote atakaye jihusisha na uhalifu ili aweze kutendewa haki.
“Tunaenda kubadilika, na upelelezi Kwa wale watakaokengeuka utakwenda haraka sana.” Alimesema Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Yesaya Sudy.
Naye, Polisi Kata wa Kata ya Buhunda, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi (A/Insp) Peter Tito pamoja na kumshukuru Kamanda Mutafungwa kwa kuitisha baraza hilo, pia ameahidi kwenda kutoa elimu zaidi ya Polisi Jamii kwa Wananchi elimu ambayo itaendelea kupunguza uhalifu kwa kiasi kikubwa kuliko kupamba na uhalifu kwani ni gharama zaidi.
Hata hivyo, mbali na maafisa wakaguzi na askari kukiri kutekeleza maelezo ya Kamanda, pia wameonesha kufurahishwa na baraza hilo kwani wamepata mwelekeo mzuri utakaowasaidia katika utekelezaji wa majukumu yao kwa mwaka 2024.