RPC: Tutatenda haki tuhuma dhidi ya Gekul

MANYARA; KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Manyara, George Katabazi amesema polisi wanachunguza tuhuma zinazomkabili mbunge wa Babati Mjini, Pauline Gekul (45) za kuhusika kumfanyia ukatili kijana aliyetajwa kwa jina la Hashimu Ally.

Kamanda Katabazi aliwaeleza waandishi wa habari kuwa walipokea taarifa kuhusu tuhuma hizo na uchunguzi unaendelea kubaini kutendeka au kutotendeka kwa jinai.

Alisema watatenda haki kwa kufanya uchunguzi kwa weledi na kwa kuzingatia maadili ya kazi ya Jeshi la Polisi.

Advertisement

“Uchunguzi bado unaendelea na pindi utakapokamilika hatua stahiki zitachukuliwa kwa mtu yeyote kwani sheria inasisitiza mtu akifanya kosa la kijinai hatua stahiki zinachukuliwa” alisema Kamanda Katabazi.

Aliongeza “Tunakaribisha wananchi kufika katika ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara kwani iko wazi kwa malalamiko yoyote, kutachukuliwa ushahidi, vielelezo vitakavyotolewa bila kuangalia hali ya mtu, tutatenda haki kwa mujibu wa sheria”

Ally alionekana katika video za mitandao ya kijamii akidai kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji na kundi la vijana kwa maelekezo ya Gekul ambaye alikuwapo katika eneo la tukio wilayani Babati.

Ally alidai Gekul aliamuru aingiziwe chupa sehemu ya haja kubwa au apigwe risasi na kwa madai kuwa alitumwa aende katika Hoteli ya Paleii Lake View Garden inayodaiwa kumilikiwa na Gekul akamwekee sumu kumdhuru kiongozi huyo.

Katibu wa mbunge huyo wa Babati Mjini (CCM), Hussein Abrima alikanusha madai kuwa Gekul alihusika kumdhalilisha Ally.

Gekul ni mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kabla ya kujiunga na chama hicho alikuwa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Gekul ambaye alikuwa Naibu Waziri wa Katiba na Sheria wakati taarifa zinasambaa, uteuzi wake umetenguliwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

 

1 comments

Comments are closed.