Rufaa ya Sabaya kusikilizwa leo

KESI ya rufaa iliyokatwa na upande wa Jamhuri kupinga kuachiwa huru aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai ole Sabaya (35) na wenzake watano inatarajiwa kuanza kusikilizwa leo.

Rufaa hiyo itaanza kusikilizwa katika Mahakama kuu Kanda ya Arusha, baada kutolewa matangazo kwa mara ya pili ya kuitwa kwa wajibu rufani wengine watano ambao wameshindwa kutokea mahakamani bila taarifa.

Kesi ya rufaa namba 155 iliyokatwa katika mahakama hiyo ilitajwa wiki iliyopita kwa ajili ya kufahamu kama hati ya wito kwa wajibu rufaa wangine mbali ya Sabaya wameitikia wito wa kufika katika mahakama hiyo kusikiliza rufaa yao, lakini hawakufika na mahakama ilitoa nafasi nyingine zaidi ya kutangaza tangazo la wito.

Wajibu rufaa ambao hawajafika katika mahakama hiyo ni pamoja na Enock Mnken, John Aweyo, Slvester Nyegu, Jackson Macha pamoja na Nathan Msuya.

Hata hivyo kwa mujibu wa sheria iwapo wajibu rufaa hawatafika leo kusikiliza kesi hiyo, itaendelea kwa aliyeko hadi mwisho na ikibainika wakata rufaa kushinda kesi hiyo, wajibu rufaa watasakwa popote walipo ili waweze kutumikia kifungo chao.

Awali Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Judith Kamala ambaye shauri hilo mara ya mwisho lilisikilizwa kwake, alisema hati ya wito ilishatangazwa katika magazeti mawili ya Desemba 17 na Desemba 20 mwaka huu.

Akimwakilisha mleta rufaa, Wakili wa Mwandamizi wa Serikali, Akisa Mhando alidai kwa kuwa tayari hati ya wito ilishatangazwa na wajibu rufaa hao hawajafika mahakamani na kuiomba Mahakama Kuu itangaze kwa mara ya pili ili wajibu rufaa hao wapate taarifa hiyo kwa mara nyingine.

Wasilisho hilo la hoja kutoka Mwanasheria Mwandamizi wa Serikali halikupingwa na wakili Faudhia Mustapher anayemtetea Sabaya, mshitakiwa wa kwanza kati wa watano wajibu rufaa.

Katika rufaa hiyo, Sabaya anatetewa na mawakili wawili Mosses Mahuna na Mustapher na wajibu rufaa wengine wanatetewa mawakili Silvester Kahunduka na Fridolini Bwemelo. Rufaa hiyo inasikilizwa na Jaji Salma Maghimbi aliyekuja rasmi kusikiliza katika Mahakama Kuu Kanda ya Arusha.

Katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha, Sabaya na wenzake waliachiwa huru na Hakimu Patricia Kisinda katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi kwa kile kilichoelezwa kuwa hakukuwa na ushahidi wowote wa kuwatia hatiani watuhumiwa.

Hakimu Kisinda mbali ya hilo, pia alisema watuhumiwa hao sita hawakupewa nafasi ya kuulizwa maswali ya dodoso kutoka kwa mawakili wao, hivyo walinyimwa haki kwa mujibu wa sheria.

Kutoka na hali hiyo, Jamhuri ilikata rufaa kupinga hukumu hiyo kwa kutoa sababu ikiwemo kuwa Hakimu Kisinda alikosea kisheria katika hukumu yake kwani ushahidi ulitolewa katika mahakama hiyo ulitosha kuwatia hatiani watuhumiwa na walipewa nafasi kisheria kuulizwa maswali na mawakili wao kama miongozo ya kisheria inavyoelekeza.

Habari Zifananazo

Back to top button