Runali waanza kugawa magunia tayari kwa msimu wa korosho

CHAMA Kikuu cha Ushirika cha Mkoa wa Lindi cha Runali kinachohudumia wilaya za Ruangwa, Nachingwea na Liwale jana kimeanza kugawa magunia ya kuhifadhia korosho ikiwa ni kujiandaa na msimu mpya wa zao hilo unaotarajiwa kuanza Oktoba 14 mwaka huu.

Meneja mkuu wa chama hicho, Jahida Hassan katika taarifa yake kwa vyombo vya habari amesema kwamba wana magunia 700,000 yanayotosheleza tani elfu 50 za korosho ambazo ndio wanatarajiwa kupata kwa msimu huu.

Alisema pamoja na kuwa na magunia hayo maandalizi mengine yakiwemo elimu na vitabu vinavyotumiwa na makarani yapo tayari.

Advertisement

Alisema ni mategemeo yake kwamba wakulima wataendelea kuleta korosho zenye ubora katika msimu ujao hasa kwa kuzingatia elimu ambayo wamepewa kuhusu uvunaji na utunzaji wa korosho kabla ya kufikisha ghalani.

Aliwataka wakulima pamoja na kuzingatia usafi wasiache korosho zao katika mifuko ya salfeti kwa kuwa inaharibu ubora wa korosho kutokana na kusababisha joto na mvuke kwenye korosho.

Akizungumza katika mahojiano hayo, Kaimu mrajisi msaidizi wa vyama vya ushirika Mkoa wa Lindi, Cesilia Sostenes alisema kwamba  kama mkoa tayari wakulima wa korosho wamepewa mafunzo kuhakikisha ubora kwani soko imara na zuri la korosho linategemea ubora wake.

Mrajisi huyo ametaka viongozi wa bodi kusimamia vizuri makarani kuhakikisha kwamba takwimu zinakuwa sawa na hakuna chnagamoto itakayojitokeza katika msimu ujao.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Hasimu Komba alisema kwamba ni matumaini yake kwamba kutakuwa na soko zuri la korosho kwa wakulima kuwasilisha korosho zenye ubora.

Alisema uchumi wa Nachingwea unategemea kilimo cha korosho hivyo akawataka maofisa ugani kutembelea wakulima wa korosho na kuona changamoto yao kabla ya msimu kuanza kutatua.

Msimu uliopita Nachingwea iliuza kilo milioni 16 za korosho kwa njia ya mnada.