“NILIWAHI kufanya kazi kwenye kampuni moja ya habari ni kubwa tu, lakini nililazimika kuacha kazi ndani ya saa 24, ili niepukane na changamoto ya usumbufu kutoka kwa baadhi ya wahariri,” anaanza kusimulia Sikudhani Chaurembo (sio jina lake halisi).
Sikudhani anasema alijiunga na kampuni hiyo ya habari akitokea Shule Kuu ya Uandishi wa Habari (SJMC) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na mara baada ya kuanza kazi alijikuta anakumbana na mishale mingi kutoka kwa mabosi zake.
“Nashukuru wazazi wangu kwa malezi ambayo walitupatia ya kuwa wawazi, kujiamini, kujituma kwenye kazi na kusimamia kile ambacho unakiamini bila kuyumbishwa, hicho kitu kwa namna moja au nyingine kimenijenga na kunifanya kuwa nilivyo leo hii.
“Wakati naingia ‘newsroom’ kuna mabosi wengi walinitaka, si unajua tena kiingiacho newsroom wenyewe wanaita usajili mpya dirisha dogo, wakati naanza kazi tayari nilikuwa na mtu wangu yeye si mwandishi yupo taasisi moja ya serikali, ambaye leo ndio baba wa watoto wangu.
“Mara zote alikuwa akiniambia maofisini kuna mambo mengi hususani anapokuja msichana mgeni kutoka chuo, mishale inayoelekezwa kwake ni mingi kwa kuwa ana kuwa na ugeni wa vitu vingi, hivyo ni jukumu lako kuikubali ikulenge au kuikwepa…; umeanza kazi jiheshimu.
“Mimi sitakuchunga maana wewe ni mtu mzima, ila madhara ya kuwa na mahusiano kazini ni mengi ikiwa ni pamoja na kuharibu kazi kwa hiyo uamuzi ni wako.
“Nakumbuka kuna siku nimetoka kwenye kazi za nje nimerudi ofisini, nikatoa ripoti ya kazi yangu kwa mkuu wangu wa kitengo, sasa wakati naandika habari yake nipo ‘busy’ nikashangaa mtu kanishika matiti, halafu kanisimamia kwa nyuma ananipapasa shingo, kiukweli nilishtuka kwa sababu sikutegemea.
“Nilipanic sana, ilikuwa ‘so embarrass’ nakumbuka nilisimama na kumzaba kibao cha uso, nadhani hata yeye hakutegemea ‘reaction’ ‘guess what’ alikuwa ni boss wangu ambaye habari naiandika yeye ndio alikuwa aipitie.
“Sasa si unajua mambo ya vyumba vya habari, mmekaa kama wodi ya hospitali kile kitendo cha mimi kureact kiliwapa watu ‘attention’, wakawa wanaangalia, yule bosi akaona aibu akaenda kukaa kwenye kiti chake hakusema kitu.
“Kuanzia hapo, alininyoosha kazi zangu akawa hatumii, akawa hanipi ushirikiano wowote, kwa sababu nilifahamu alikuwa anafanya vile kwa sababu zipi haikunisumbua sana, nilichofanya nikawa sitegemei habari yangu itoke kwake, nikawa naandika habari zote makala zaidi.
“Baadae akahamishwa dawati, nikadhani labda nitapumua, lakini haikua hivyo, nilijikuta napita kwenye kipindi kigumu zaidi, kwa bosi ambaye aliachwa kukaimu nafasi ya aliyehamishwa.
“Mwanzo alianza kwa kunikandamiza unaandika habari hazitoki, ukiwa na habari kubwa atakwambia nielezee yote yaliyoongelewa, ukimuelezea anakwambia tunayo, halafu anaiandika yeye na kumpa ‘byline’ mtu mwingine.
“Au anakwambia andika, unaandika unampa, anatoa ‘byline’ yako mbaya zaidi unakuta anaweka ‘byline’ ya mtu mwingine, ukiuliza anakwambia fulani alikuwa nayo, utamuhoji sasa mbona uliniambia niandike? Na je huyo fulani ‘art’ yake tunafanana? Kuanzia intro nilivyoandika mpaka nukta kiboko kabisa…
“Nikajikuta naingia kwenye mgogoro mkubwa sana na huyo kaimu, mwisho wa siku, akaamua kunifungukia.
“Aliniita kwenye kantini ya ofisi akaniambia, Sikudhani wewe ni binti mrembo sana, lakini tatizo lako unakaza sana ndio maana maisha yako hapa ofisini yanakuwa magumu, kila anayekuja kwako ili aonje asali yako unabana.
“Kiukweli nilibaki namtolea macho nikamuliza ndiyo kitu ulichoniitia bosi? Akasema hapana hiyo nimechomekea tu, nikamuliza umeniitia nini? Akasema kaa basi kwanza mbona umesimama wima wima, nikakaa, akaniambia unajua ni muda mrefu sasa nimekuonesha dalili zote kuwa nakuhitaji, lakini hauoneshi ushirikiano, sign zote huzielewi kwa hiyo mimi nasikia hasira ndio maana nimekuwa nikikukomoa.
“Sasa naomba nikueleze yaliyopo moyoni mwangu, mimi nakupenda sana, iwapo utanikubalia, ‘assignment’ zote kubwa nitakuwa nakupanga, utaenjoi maisha ya ofisini, nikamuliza kwa ukali unasemaje?
“Akajibu aah Sikudhani ina maana hujanielewa, wewe si mtu mzima? kiukweli nilisikia kutetemeka, hasira zikanipanda, nikasema huyu ananichukuliaje yaani, yaani mimi niuze utu wangu kwa ajili ya kupangiwa ‘assignment’ kubwa, kwanza ananionaje, nilichomjibu kamwe siwezi kutembea na yeye na si yeye tu bosi yeyote kwa ofisi ile nikanyanyuka na kuondoka.
“Sasa sijui wahariri huwa wanaambiana au la, ile kila mtu anajaribu bahati yake, maana baada ya siku moja akaniibukia mhariri mwingine, yeye alinieleza wazi nikamwambia sikutaki, akaniuliza hivi unachoringia ni nini? Kila mtu humtaki unajiona keki sana, nikamwambia kama sio keki mnaifuatia nini? mnadhani kila mtu maharage ya Mbeya, akatoka hapo akaenda kwa HR akamwambia mfukuze kazi Sikudhani.
“HR ni mwanaume lakini ni baba mstaarabu sana akamuuliza nimfukuze kwa sababu gani? Hana sababu, akamwambia nipe ushahidi wa kosa lolote alilolifanya ambalo linastahili kumfukuza kazi ukiniletea nitamfukuza, akakosa ushahidi.
“Sasa HR akaniita akaniambia una ugomvi na fulani nikamwambia hapana, akasema kaja hapa kaniambia hivi na vile, nilijikuta tu nasikia hasira nikatoka nikaenda kuandika barua ya kuacha kazi mimi mwenyewe ndani ya saa 24.
“Nikaipeleka kwa HR akaisoma akaniambia una kichaa? yaani uache kazi kwa ajili ya ‘issue’ ndogo kama hizi, tena unaacha ndani ya saa 24 nikamuelezea yote niliyokuwa nayapitia kwa wakati huo akasikitika akasema mbona siku zote hukuwahi kuja kusema?
“Akaichana ile barua yangu ya kuacha kazi akaniambia changamoto hazikimbiwi unatakiwa kukabiliana nazo, nikamwambia siwezi tena, nilipofika imetosha, nikaenda kuprinti barua nyingine na kumkabidhi tena HR kisha nikaondoka, hapo ikawa mwisho wa mimi na hiyo kampuni,” anasema Sikudhani.
Huyo ni Sikudhani mmoja ambaye ameamua kuvunja ukimya na kuweka wazi yaliyomkimbiza kwenye uandishi wa habari, fani ambayo anasema awali aliipenda sana, lakini aliyokutana nayo hatamani hata ndugu yake mmoja aingie kwenye fani hiyo.
UTAFITI WA TAMWA
Ripoti ya utafiti wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA), inaeleza asilimia 52 ya waandishi wa habari Tanzania hawapo tayari kuweka wazi kuhusu manyanyaso ya rushwa ya ngono wanayoyapata kazini.
Utafiti huo uliofanyika Dar es Salaam, ripoti hiyo inabainisha ni asilimia 48 ambao wanaweza kujieleza kuhusu manyanyaso hayo.
Ni utafiti ambao ulihusisha waandishi wa habari wa kujitegemea, wenye mikataba midogo na waliopo mafunzoni, wahariri wakuu na wahariri waandamizi, maofisa uajiri, vyuo vya habari na asasi za kiraia.
Utafiti huo ulibaini zipo sababu kadhaa ambazo zinachangia tatizo la rushwa ya ngono si tu kwa waandishi, bali vyuoni na sehemu nyingine mahala pa kazi.
Mkurugenzi wa Tamwa,Dk Rose Reuben akizungumza na HabariLEO anasema sheria ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ya Mwaka 2007, Kifungu cha 25 inafafanua kinagaubaga kwa kutofautisha rushwa ya ngono na rushwa nyingine.
“Kimantiki, sheria hii inakiri kuwa, rushwa ya ngono inatokana na matumizi mabaya ya mamlaka; pale mwenye mamlaka (mwanaume au mwanamke) anapotumia nafasi yake kushawishi, kudai na kulazimisha kutoa haki kwa sharti la ngono,” anasema.
Anasema kupitia tafiti waliyofanya, wanapata mrejesho mkubwa kuwa rushwa ya ngono imechukua hatamu sehemu za kazi na kwenye taasisi za elimu ya juu.
“Nilihudhuria mkutano mmoja wa Chama cha Wakandarasi Wanawake Tanzania (TWCA), kule pia hali si nzuri ili kupata zabuni inabidi watoe rushwa ya ngono na wakati mwingine mtu anatoa ngono na tenda hapati,”anasema.
AHADI HUWAINGIZA TAMAA
Stumai John (sio jina lake halisi) anasema wapo baadhi ya wanawake maofisini huingiwa tamaa kutokana na ahadi wanazopewa ikiwemo kupandishwa vyeo, kwa wanaojitolea kupata nafasi ya kuajiriwa, kupewa vipaumbele katika vitu fulani fulani, hivyo hukubali, mwisho wa siku wanashindwa kufikia malengo yao.
“Kwa sababu, unaweza kweli ‘kugongwa’, ukapata ulichoahidiwa, na unaweza ukageuzwa shamba la bibi ukafanywa mpira wa kona, wanaume wana tabia ya kuambiana, umemkubalia mmoja anakwenda kuwaeleza wenzake, anakuja mwengine na mwengine tena kukutongoza,” anasema.
Spika wa Bunge Dk. Tulia Ackson aliwahi kuwafunda wanafunzi wa kike wa vyuo na kuwataka kuwa na ujasiri wa kukabiliana na changamoto za maisha, badala ya kuuza miili yao na kupunguza thamani ya utu wao.
Akasema kama wanawake wanaotaka kwenda mbele zaidi wanatakiwa kuthamini utu wao badala ya kujiingiza katika rushwa ya ngono.
Akasema, ili wanafunzi wa kike na wanawake kwa ujumla waweze kuepukana na tatizo la rushwa ya ngono hata katika chaguzi za ndani ya vyama vya siasa, ni lazima wawe na misimamo pamoja na kujiamini katika kile wanachokifanya
KAGUENI VYETI SI MAUNGO
Mwakilishi wa Mtandao wa Ushirikishaji Wanaume ‘Men Engage’ Dk Katanta Simwanza akizungumza na HabariLEO, anasema wanaume mahala pa kazi wanapaswa kuwa sehemu ya mapambano ya kupinga rushwa ya ngono kuwa wao ndiyo wafanyaji wa vitendo hivyo kwa asilimia kubwa.
“Wanaume tunapawa kujua kwamba rushwa ya ngono inaathiri utendaji na hata kuua ndoto za wanawake wengi, hebu kazi yetu iwe kukagua vyeti na sio maungo,”amesema.
Dk Katanta anasema baadhi yao wanatumia madaraka vibaya sehemu mbalimbali kwa kuwapandisha vyeo kwa ajili ya rushwa hali ambayo inaondoa utu wa kupanda kwa vyeo hivyo.
Mwakilishi wa ubalozi wa Canada Pamela O’ Donnell, amesema kuwa rushwa ya ngono ipo duniani kote hivyo mapambano hayo ni ya dunia nzima katika kupaza sauti.
Kwa upande wa Mkrungenzi wa Taasisi ya Wanawake katika Jitihada za Kimaendeleo (WAJIKI), Janeth Mawinza, anasema kwa ufadhili wa WFT-T, wameanzisha na kuimarisha klabu za kupinga rushwa ya ngono na vitendo vya ukatili wa kijinsia katika sehemu mbalimbali mkoani Dar es Salaam.
Anasema, Wajiki inaendesha kampeni ya ‘Safari Salama Bila Rushwa ya Ngono kwa Wasichana na Wanafunzi Inawezekana’, inayolenga kuwajengea uwezo wanaume ili wabadilike na kuwa walinzi wa usalama kwa wasichana na wanawake.
Naye mlezi wa Sauti ya Jamii Kipunguni, Ilala Dar es Salaam, Seleman Bishagazi, anasema elimu zaidi kwa jamii inahitajika.
Anasema utafiti waliofanya kwa wahudumu wa baa katika baadhi ya mikoa walibaini wahudumu wa kike kudhalilishwa kwa kushikwa maungo yao wanachukulia ni jambo la kawaida.
“Mkoani Singida katika baa moja muhudumu wa kike aliyekuwa anawahudumia akasema “Hata mteja (mwanaume) anishike matiti au sehemu yoyote nikiwa kazini nahudumia, hakuna tatizo, shida ni mtu kunifanyia hivyo nje ya mazingira ya kazi…”
“Mkoani Arusha, tulibaini kuwa, mgambo hudai rushwa ya ngono kwa wanawake wafanyabiashara ili wasiwabugudhi wanawake hao wanapofanya biashara katika maeneo yasiyoruhusiwa… Kubwa zaidi ambalo ni tatizo, wanawake wengi hawawaambii waume zao changamoto hizi kwa kuwa wanahofia kupata misukosuko ya kutoaminiwa na mume…”
Anasema kwa uchungu: “Kosa kubwa kwa Tanzania na nchi za Afrika Mashariki ni kwamba, hatubebi thamani ya mwanamke na bila kujua, tunazidi kupata hasara… Angalia hata pale Ukonga (Dar es Salaam) watoto wa kike mpaka sasa wanakeketwa. Ni ajabu sana…”
Comments are closed.