RAIS Mteule wa Kenya, Dk William Ruto amesema amezungumza kwa simu na Rais anayemaliza muda wake, Uhuru Kenyatta.
Ruto alieleza hayo Jumatano zikiwa zimepita siku kadhaa tangu aseme hajazungumza na Rais Kenyatta kwa miezi kadhaa.
Mwanzoni mwa wiki hii, Mahakama Kuu ya Kenya ilithibitisha ushindi wa Ruto baada ya mpinzani wake, Raila Odinga kufungua kesi katika mahakama hiyo kudai kuwa kulikuwa na udanganyifu katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, mwaka huu.
Baada ya kuthibitishwa na mahakama hiyo, Ruto alisema Kenyatta ni rafiki yake na aliahidi kumpigia simu Rais Kenyatta kwa kuwa walikuwa hawazungumzi kwa miezi kadhaa.
Kupitia ukurasa wake katika mtandao wa kijamii wa twitter, Ruto alieleza kuwa alizungumza na bosi wake yaani Rais Kenyatta kwa njia ya simu.
“Tulijadiliana kuhusu uchaguzi mkuu uliomalizika hivi karibuni na kubadilishana madaraka kwa kuzingatia mila na desturi zetu za kidemokrasia,” alisema Ruto.
Akizungumza baada ya kuthibitishwa na Mahakama Jumatatu iliyopita, Ruto alisema alipoamua kumuunga mkono Kenyatta kuwa Rais wa nchi hiyo hakufanya hivyo kwa masharti kwamba Kenyatta naye aje amuunge mkono.
Alisema hana kinyongo kwamba Rais Kenyatta aliamua kuchagua na kumuunga mkono mtu mwingine yaani Odinga hivyo wataendelea kuwa marafiki.
Aidha, vyombo vya habari nchini humo vimeripoti kuwa Rais mteule Ruto anatarajiwa kuapishwa siku ya Jumanne ijayo ya Agosti 13 kuwa Rais wa tano wa Kenya na maandalizi yanaendelea vizuri.