RAIS wa Kenya Dk William Ruto ameunga mkono wito wa kufanyia mapitio Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), akisisitiza kuna maeneo mbalimbali ambayo yanahitaji kupitiwa upya.
“Ni wakati wa kuangalia mkataba, hasa kuhusu lugha zinazotumiwa katika Bunge la Afrika Mashariki (EALA).
Bila shaka, Kiswahili kitaendelea kuwa na jukumu kubwa katika Bunge hilo,” Ruto alisema.
Ruto alikuwa akijibu ombi la Spika wa EALA, Joseph Nkakirutimana la kufanyia marekebisho Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Nkakirutimana na wajumbe wengine walikuwa wamealikwa na Rais Ruto katika Ikulu ya Nairobi.
Katibu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Rebecca Miano pia alikuwepo Ikulu kwa mkutano huo, huku Spika akiambatana na Wabunge wa Kenya EALA, Hassan Omar, Kanini Kega na Zipporah Kering na Naibu Mkurugenzi wa EALA John Mutega.
Rais Ruto alisema kuwa kuna kazi imeanza kuhusu umuhimu wa kulipa Bunge la EALA uhuru wa kifedha kama mabunge mengine ya kikanda.
“Baraza la Mawaziri linachunguza suala hilo na limewapa jukumu la kuandaa mpango, Sekretarieti ya EAC,” alisema.