Ruto azuru Tanzania

RAIS wa Jamhuri ya Kenya, Dk William Ruto amewasili nchini jana jioni kwa ziara ya kikazi ya siku mbili. Hii ni ziara ya kwanza ya Dk Ruto nchini baada ya kushinda Uchaguzi Mkuu uliofanyika Agosti 9 mwaka huu.

Jana kabla ya kuja nchini alihudhuria sherehe za miaka 60 ya Uhuru wa Uganda iliyofanyika katika viwanja vya Kololo jijini Kampala.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Stergomena Tax aliongoza viongozi wa serikali kumpokea Rais Ruto na ujumbe wake akiwemo mkewe, Rachel Ruto kwenye Kiwanja cha Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam.

Taarifa ya kitengo cha Mawasiliano Serikalini katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ilieleza kuwa leo Dk Ruto atakwenda Ikulu ya Dar es Salaam kuzungumza na mwenyeji wake, Rais Samia Suluhu Hassan.

Baada ya mazunguzo hayo, Dk Ruto na Rais Samia wanatarajiwa kuzungumza na waandishi wa habari na baadaye watashiriki dhifa ya kitaifa aliyoiandaa Rais Samia Suluhu Hassan.

Taarifa hiyo kwa umma ilieleza kuiwa baada ya dhifa hiyo, Dk Ruto na ujumbe wake wanatarajiwa kuondoka nchini kurejea Kenya.

Mei 4 na 5 mwaka jana, Rais Samia alifanya ziara ya siku mbili Kenya na nchi hizo zikakubaliana kuboresha mazingira ya biashara ikiwa ni pamoja na kuondoa vikwazo ili kushirikiana badala ya kushindana kibiashara na kuongeza uwekezaji wa pamoja kwa faida ya uchumi wa nchi hizo na watu wake.

Rais Samia na mwenyeji wake, Uhuru Kenyatta walitoa msimano huo jijini Nairobi wakati wa Jukwaa la Wafanyabiashara wa Kenya na Tanzania. Rais Samia, alisema walizungumza na Rais Kenyatta na kukubaliana kwamba, nchi hizo zinapaswa kushirikiana kibiashara na kwamba, Tanzania ipo tayari kwa hilo.

“Tanzania ipo tayari kupokea wawekezaji kutoka Kenya kwa mikono miwili na milango iko wazi kushirikiana katika eneo hilo. Serikali ipo tayari na itakuwa ni zaidi ya daraja kuwezesha hili kufanikiwa kwa manufaa ya nchi zetu mbili,” alisema Rais Samia.

Walipozungumza na waandishi wa habari jijini Nairobi, Rais Samia alimuahidi Uhuru kwamba Tanzania itaendelea kukuza na kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizo mbili na imejipanga kuwekeza nchini humo. Alisema Kenya imewekeza miradi 513 yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 1.7 ambayo imetoa ajira zipatazo 51,000 kwa Watanzania.

Rais Samia alisema zipo kampuni 30 za Kitanzania ambazo zimewekeza mtaji nchini Kenya wenye thamani ya shilingi za Kenya bilioni 19.330 iliyotoa ajira kwa watu 2,640.

Kenya ni miongoni mwa washirika wakubwa wa kibiashara wa Tanzania ikiwakilisha takriban asilimia 4.3 ya bidhaa zote za Tanzania zinazouzwa nje na asilimia 4.1 ya bidhaa zinazoagizwa kutoka Kenya. Katika kipindi cha miaka mitano Tanzania na Kenya zimefanya biashara yenye thamani ya wastani wa Sh trilioni moja za Kitanzania.

Kwa mujibu wa takwimu za Baraza la Biashara la pamoja la nchi hizo mbili (Tanzania na Kenya), takribani kampuni 550 za Kenya zinaendesha shughuli za kibiashara nchini Tanzania na makadirio ya mwaka wa 2016 yalionesha kwamba kampuni hizo zilikuwa zimewekeza jumla ya kiasi cha Dola za Marekani bilioni 1.7 nchini Tanzania na kutoa ajira kwa Watanzania takribani 56,260.

Baada ya kuapishwa, Rais Ruto alisema vipaumbele katika sera yake ya mambo ya nje kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ni kuendeleza ushirikiano wa kidiplomasia, kibiashara na kudumisha amani, utulivu na mshikamano miongoni mwa nchi wanachama.

Alisema serikali yake itaendeleza uhusiano wa kirafiki, kibiashara na diplomasia na majirani zake na kuhakikisha amani na utulivu vinatamalaki katika nchi zote za Afrika Mashariki.

Habari Zifananazo

Back to top button