Ruto kuapishwa leo, aahidi amani, ushirikiano EAC

RAIS Mteule wa Kenya, Dk William Ruto anaapishwa leo katika sherehe zinazotarajiwa kufanyika katika Viwanja vya Kasarani mjini Nairobi na kuhudhuriwa na wakuu wa nchi, wageni mbalimbali pamoja na wananchi wanaokadiriwa kufikia 60,000.

Katika hafla hiyo wakuu wa nchi 20 wanatarajiwa kuhudhuria wakiwemo Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Viongozi hao ni pamoja na Rais Samia Suluhu Hassan, Rais Yoweri Museveni wa Uganda, Rais Paul Kagame wa Rwanda na Rais Evariste Ndayishimiye wa Burundi.

Kuapishwa kwa Ruto kutaanzisha zama nyingine mpya za uongozi nchini Kenya. Tayari Ruto ameeleza sera yake ya Mambo ya Nje na kutaja vipaumbele vya serikali yake katika EAC.

Vipaumbele hivyo ni pamoja na kuendeleza ushirikiano wa kidiplomasia, kibiashara pamoja na kudumisha amani, utulivu na mshikamano miongoni mwa nchi wanachama wa jumuiya hiyo ya kikanda.

Alisema katika Sera yake ya Mambo ya Nje, hakutakuwa na mabadiliko makubwa kama ilivyo kwa mtangulizi wake Rais anayeondoka wa Awamu ya Nne, Uhuru Kenyatta, akiongeza kuwa atakachofanya ni kuiboresha mahali penye mapungufu.

Dk Ruto alisema Muungano wa Kenya Kwanza utafanya kila liwezekanalo kuhakikisha kuwa Kenya inaendelea kuwa mhimili wa amani na utulivu katika mataifa yote ya Afrika Mashariki kama ilivyofanya serikali inayoondoka madarakani katika kipindi chake cha miaka 10.

Balozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) nchini Kenya, Francine Muyumba alisema nchi yake imefurahishwa na kauli ya Rais Mteule kwa sababu Kenya kupitia kampuni zake inachangia katika ukuaji wa uchumi wa DRC.

“Si tu kuwa Kenya imepata soko kubwa la kuuza bidhaa zake baada ya DRC kujiunga na EAC, bali pia kampuni kadhaa za Kenya kama Equity Group na KCB yanaendelea kuchangia ukuaji wa uchumi wa Congo,” aliongeza Muyumba.

Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Biashara la Afrika Mashariki ambaye pia ni Kiongozi wa Sekta Binafsi nchini Uganda, Simon Kaheru, alisema maneno ya Rais Mteule yanaonesha kuwa yuko tayari kufanyia kazi changamoto za kibiashara na uwekezaji ndani ya Afrika Mashariki.

 

 

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button