Ruto kuhutubia wabunge, maseneta

RAIS William Ruto anatarajiwa kuhutubia wabunge wa Bunge la Kitaifa na Bunge la Seneti katika kikao cha pamoja Alhamisi hii.

Katika taarifa iliyochapishwa magazetini, Spika wa Bunge la Kitaifa, Moses Wetangula na Spika wa Seneti, Amason Kingi, walisema Rais Ruto atakuwa akitoa hotuba yake ya kuzindua Bunge kwa mujibu wa Kifungu cha 132 (1) (a) cha Bunge cha Katiba.

Kenya ilifanya Uchaguzi Mkuu Agosti 9, mwaka huu. Miongoni mwa nafasi zilizofanyiwa uchaguzi ni urais, ubunge na useneta.

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), ilimtangaza Dk William Ruto kuwa mshindi wa kiti cha Urais, lakini mpinzani wake wa karibu, Raila Odinga alikimbilia mahakamani kupinga ushindi huo. Hata hivyo, mahakama ya upeo nchini hapa ilimthibitisha Ruto kuwa mshindi halali wa kiti hicho hivyo, akaapishwa kuwa Rais wa Tano wa Kenya akichukua nafasi ya Uhuru Kenyatta aliyemaliza muda wake.

Wabunge na maseneta wote wanatarajiwa kuhudhuria kikao hicho kitakachoanza saa 2:30 usiku.

Hotuba ya rais inajiri baada ya wabunge hao kufanya utambulisho wa wiki moja katika Hoteli ya Safari Park jijini Nairobi (Wabunge) na katika Sawela Lodge huko Naivasha (Maseneta).

Katika mwelekeo huo, wabunge hao walielezwa majukumu yao, hali ya uchumi na diplomasia.

Pia walipewa mafunzo kuhusu kanuni na taratibu za bunge, usalama, utungaji wa sheria, mchakato wa kutengeneza bajeti na fedha za umma.

Kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge, wabunge hao lazima wachukuliwe hatua ya kujitambulisha kabla ya kuanza vikao vyao rasmi.

 

Habari Zifananazo

Back to top button