Ruvuma wajipanga utalii wa kiutamaduni

WADAU wa utalii Mkoa wa Ruvuma wanakusudia kuanzisha na kukuza utalii wa kiutamaduni (cultural tourism) sanjari na kuboresha maeneo yote ya kihistoria, ili kuendeleza utamaduni na kuingiza mapato kupitia utalii.
Hayo yamesemwa na Ofisa Maliasili na Utalii wa Mkoa wa Ruvuma, Afrikanus Challe leo Januari 19, 2023 na kuongeza kuwa nia yao ni kuhakikisha mkoa huo unapata watalii na kukuza uchumi kama.
Alisema wadau hao wameshatembelea baadhi ya maeneo muhimu ya kihistoria mkoani humo ikiwemo Makumbusho ya Taifa ya Majimaji, Makumbusho ya Rashid Kawawa, Maposeni, Luhira, Peramiho na Chandamali Wilaya ya Songea, ili kutambua maeneo ya kihistoria na umuhimu wake kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.
“Huu ni mwanzo wa jukumu la kuziboresha kumbukumbu za kihistoria Mkoa wa Ruvuma na kuimarisha utalii wa ndani na nje, lengo likiwa ni kuutangaza mkoa wa Ruvuma,’’ amesisitiza Challe.
Kwa upande wake Mhifadhi Kiongozi wa Makumbusho ya Taifa ya Majimaji, Bartazar Nyamusya amesema serikali imedhamiria kuyafanya Makumbusho ya Taifa ya mashujaa wa vita ya Majimaji kuwa makumbusho ya mfano nchini kutokana na kuhifadhi vifaa halisi na silaha halisi, ambazo zilitumiwa na mashujaa kupambana na wakoloni wa Kijerumani.
“Hii ni Makumbusho pekee nchini iliyoanzishwa mwaka 1980 ambayo imebahatika kuwa na vifaa vyote asilia na muhimu katika utamaduni na historia ya Mtanzania, hali ambayo inaitofautisha makumbusho hii na nyingine zilizopo hapa nchini,” alisisitiza Mhifadhi huyo.