Rwanda kuimarisha soko la chai kimataifa
RAIS Paul Kagame amesema serikali yake itaendelea kushirikiana na wakulima wote nchini kuhakikisha inaimarisha soko la kimataifa la mazao ikiwemo chai, kahawa, maparachichi pamoja na bidhaa za ngozi kutoka kwa wafugaji.
Kiongozi huyo aliyasema hayo wakati wa kuhitimisha ziara yake iliyochukua wiki nzima katika maeneo mbalimbali ambapo alipata fursa ya kutembelea kiwanda cha chai, ranchi za ufugaji, mabwawa ya uzalishaji wa umeme na wafanyabiashara wadogo mjini Kigali.
Kagame aliahidi kuongeza msaada katika sekta ya kilimo ili kuongeza uzalishaji akiongeza kuwa sekta ya kilimo ndiyo inayoongoza kwa kutoa ajira nyingi kwa wananchi wa Rwanda. Alisema uzalishaji katika sekta ya kilimo utakuwa chachu ya kuimarisha sekta ya viwanda ambayo inategemea kilimo.
“Sote tunajua kuwa tukiimarisha sekta ya kilimo kwa kutoa ruzuku katika kilimo kama pembejeo za kilimo, mbolea na mbegu ni dhahiri kuwa tutakuwa tumeimarisha sekta ya kilimo ambayo inachangia asilimia kubwa ya ajira za wananchi wa Rwanda,” alisema Kagame.
Kilimo cha chai kilianzishwa nchini Rwanda miaka ya 1950, mpaka mwishoni mwa mwaka 2021 kulikuwa na hekta zaidi ya 26,000 za mashamba ya chai nchini Rwanda. Kwa mujibu wa Bodi ya Chai ya Rwanda, uzalishaji wa chai umekuwa ukiongezeka kila mwaka.
Mwaka 1980, Rwanda ilikuwa ikizalisha tani 5,910 za chai, mwaka 1990 ikawa inazalisha tani 12,855 na hadi kufika mwaka 2021 Rwanda ilizalisha tani 36,000 za chai kwa mwaka na kuingiza kiasi cha dola za Marekani milioni 103.