MATAIFA ya Rwanda na Uganda yameanzisha tena mazungumzo rasmi ya kidiplomasia yenye lengo la kurudisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili ambazo hazikuwa na uhusiano mzuri kwa muda mrefu.
Ujumbe wa Serikali ya Uganda ulioongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa taifa hilo, Odongo Abubakhar uliofika nchini wiki iliyopita na kupokewa na wenzao wa Rwanda, walifanya mazungumzo mjini Kigali wikiendi iliyopita.
Wajumbe wengine waliokuwemo katika ujumbe huo wa Uganda ni pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje, Bagiire Waiswa na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Kanda na Masuala ya Kisiasa ya Kimataifa, Arthur Kafeero.
Mbali na wajumbe hao, Balozi Mteule wa Uganda nchini Rwanda, Robert Rusoke alikuwepo pia katika mazungumzo na ujumbe wa Serikali ya Rwanda ukiongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Vincent Biruta.
“Mawaziri walibadilishana mawazo kuhusu masuala ya kikanda yanayohusu usalama, biashara, uwekezaji pamoja na miradi ya kimkakati ya kikanda. Walikubaliana kudurusu uhusiano na ushirikiano katika maeneo mbalimbali katika kikao kijacho kati ya Rwanda na Uganda,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.