Saba watinga nusu fainali riadha Afrika

WACHEZAJI saba wa timu ya Taifa ya riadha chini ya umri wa miaka 18 na 20 wametinga hatua ya nusu fainali ya mashindano ya Afrika yanayoendelea Ndola, Zambia.

Kwa mujibu wa kocha wa timu hiyo Alfredo Shahanga, kati ya wanariadha nane, saba wamefuzu kucheza nusu fainali.

Walioingia ni Mpaji Lukindo meta 400  wa U-18 akitumia sekunde 49.8 kwa wanawake meta 100 ni Nasra Abdallah akitumia sekunde 12.5 na Berther Ernest kwa sekunde 12.74.

Kwa wanaume meta 100 chini ya miaka 18 ni Alex Sezario akitumia sekunde 11.4, Said Alli  sekunde 11.4, Benedicto Mathius wa U-20 alitumia  sekunde 11.2 na Gasisi Geagasa wa U-20 alitumia sekunde 11.12.

Baada ya matokeo hayo, timu ya Tanzania jana ilitarajia kuingia uwanjani katika michezo ya miruko na mitupo katika mbio za kuwania medali ya mashindano hayo ambayo ni sehemu ya kufuzu kwa mashindano ya dunia.

Timu ya Tanzania ina wachezaji 15 wanawake na wanaume kwenye mashindano hayo ambayo yalianza Aprili 27 na yanatarajiwa kumalizika Mei 3 mwaka huu.

Habari Zifananazo

Back to top button