Sababu ndege nyingi kuja Tanzania zatajwa

MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Hamza Johari amesema kufungwa kwa mitambo ya kisasa zikiwemo rada mpya katika viwanja vya ndege nchini, kumefanya anga la Tanzania kuwa salama na kuvutia mashirika ya kimataifa ya usafiri wa ndege kuja nchini.

Johari alisema hayo Alhamis  Dar es Salaam katika ufunguzi wa mkutano wa 12 wa Shirikisho la Wahandisi wa Mitambo ya Kuongoza Ndege Afrika (IFATSEA), unaofanyika jijini humo kwa siku nne na kushirikisha nchi zaidi ya 15 za Afrika.

Alisema katika sekta ya usafiri wa anga moja ya eneo muhimu ni mitambo ya kuongoza ndege ambayo hutumiwa na wahandisi wa taaluma hiyo kuziongoza ndege wakati wa kuruka na kutua salama.

“Tanzania tuko vizuri, tumefunga rada mpya za kisasa na tuna wataalamu wa mitambo ya kuongoza ndege wa kutosha. Hii inatufanya tuaminike kimataifa na hata mashirika ya kimataifa ya ndege yanaangalia moja ya kigezo hicho kuleta ndege zao kwetu,” alisema Johari.

Alisema TCAA kila mwaka hutenga asilimia 20 ya bajeti yake kwa ajili ya mafunzo kwa wataalamu wake.

Hatua hiyo alisema imeifanya TCAA kuaminiwa na nchi wanachama wa masuala ya usafiri wa anga na kuomba wataalamu wake katika fani za usafiri wa anga kwenda kutoa mafunzo katika nchi hizo.

Alisema lengo la mkutano huo ni kuwakutanisha wahandisi wataalamu wa mitambo ya kuongoza ndege ya angani na ardhini ili wazungumze changamoto zao na kuzipatia ufumbuzi kwa lengo la kuhakikisha sekta hiyo inafanya kazi salama muda wote.

Alisema matamanio yao ni kushirikishana zaidi masuala ya teknolojia ya kisasa katika sekta hiyo kwa sababu ni eneo ambalo kila mara kunakuwa na mabadiliko ya teknolojia na mitambo mipya.

“Tuko vizuri kwenye eneo la mafunzo na hii inatusaidia hata kusaidia wenzetu kuwapa wataalamu kwenda kutoa mafunzo kwao na hii inatujenga na sisi tunakua katika sekta ya usafiri wa anga na kupanda nafasi za ubora katika Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO),” alisema Johari.

Awali akifungua mkutano huo, Mkurugenzi wa Huduma za Usafiri wa Anga katika Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Aron Kisaka alisema ni muhimu waongoza ndege Afrika kukutana, kujadiliana na kuelezea changamoto za sekta hiyo na kuzipatia ufumbuzi.

Rais wa Chama cha Wahandisi wa Mitambo ya Kuongozea Ndege Tanzania (TATSEA), Francis Chale alisema wanashiriki mkutano huo wa 12 ili kutathmini kazi zinazofanywa na wahandisi hao barani Afrika kwa ajili ya kuangalia mabadiliko ya teknolojia mpya katika sekta hizo ili kwenda na wakati.

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button