MATATIZO ya afya ya akili ni miongoni mwa changamoto zinazowasumbua watu wengi kwa sasa katika jamii.
Matumizi ya dawa za kulevya, msongo wa mawazo na hali ngumu ya maisha ni miongoni mwa sababu za tatizo hilo. Wanaume ni kundi linalotajwa kuathirika zaidi.
Wataalamu wa afya ya akili wanasema wanaume wanaweza kupata tatizo hilo mara mbili zaidi ya wanawake.
Wanasema wanaume wanawahi haraka kupata matatizo ya afya ya akili katika umri mdogo kulinganisha na wanawake lakini kwenye sonona uwiano unaweza kuwa sawa.
Hamza Jabir (jina si halisi) ni mwanaume aliyewahi kupata ugonjwa wa akili kutokana na matumizi ya dawa za kulevya.
Hamza aliingia katika matumizi ya dawa za kulevya baada ya kufika Dar es Salaam na kukutana na marafiki ambao wanatumia dawa hizo kwa kuwa alikuwa na msongo wa mawazo uliosababishwa na hali ngumu ya maisha.
“Mimi ni mzaliwa wa Shinyanga, nilikuja Dar es Salaam nikiwa na miaka 18 kutafuta maisha, nilikuwa nakaa na ndugu yangu ambapo baadaye nilishindwa kuelewana nao ikabidi nihamie kwa marafiki,” anasema Hamza.
Alifikiri ni suluhu ya matatizo yake kutumia dawa za kulevya lakini ikawa tofauti.
“Nilianza kuwa teja, nilikuwa nikifanya kazi kampuni moja hapa mjini lakini niliachishwa kazi,” anasema Hamza.
Anasema tayari alishakuwa mraibu wa dawa za kulevya na hakuwa na jinsi ya kutoka katika hali hiyo.
“Ndugu zangu wakanichukua na kunileta Hospitali ya Taifa Muhimbili kupata huduma za methadone (dawa ya kupunguza au kuondoa utegemezi wa dawa za kulevya) na naendelea vizuri sasa ninaona mabadiliko na watu wanaonizunguka wanaona mabadiliko ya tabia zangu,” anasema.
Hamza anawashauri vijana hasa wa kiume wajiweke mbali na matumizi ya dawa za kulevya kwani haziwezi kutatua changamoto walizonazo bali zitawaingiza katika matatizo ya afya ya akili.
WANAUME VINARA
Licha ya juhudi za kupunguza tatizo la magonjwa ya akili, tatizo bado ni kubwa kwa wanaume kuliko kwa wanawake.
Kwa mujibu wa takwimu za Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), mwaka 2019/20 wagonjwa wa afya ya akili 33,287 walitibiwa katika hospitali hiyo ikiwa ni ongezeko la asilimia 34.1 kutoka wagonjwa 21,936 waliorekodiwa mwaka 2018/19.
Wagonjwa hao wa akili walitibiwa katika vituo viwili vya hospitali hiyo vya Upanga na Mloganzila.
MNH inaeleza kuwa mwaka 2020/21 kulikuwa na ongezeko la asilimia 17 la wagonjwa wa akili waliotibiwa hospitalini hapo huku idadi kubwa ikiwa ni wanaume.
Pia mwaka huo, kati ya wagonjwa wa nje 24,014 waliotibiwa, wanaume walikuwa 15,205 sawa na asilimia 63.3 sawa na kusema kuwa kwa kila wagonjwa 10 wa nje wa magonjwa ya akili waliotibiwa Muhimbili, zaidi ya nusu au sita walikuwa wanaume hasa vijana.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), mwaka 2019, mtu mmoja kati ya wanane anakabiliwa na matatizo ya ugonjwa wa akili.
WHO inaeleza kuwa magonjwa ya akili huwapata zaidi wanaume kutokana na mazingira wanayoishi.
SABABU WANAUME KUPATA MAGONJWA YA AKILI
Mtaalamu wa Saikolojia kutoka Chuo cha Kikatoliki cha Mwenge (MWECAU), Christian Bwaya anasema ni kweli kuwa wanaume wanakumbwa na tatizo hilo kutokana na mfumo wa maisha katika jamii.
“Hata wanaojaribu kujiua au kuua kwa wingi ni wanaume, kweli tatizo ni kubwa,” anasema Bwaya.
Anasema wanaume wengi wanaweka vitu moyoni na si rahisi kuweka wazi mambo yao, hivyo kuwa katika hatari zaidi ya kupata matatizo ya afya ya akili.
Hali hiyo ndiyo inayoathiri afya ya akili kwa wanaume wengi na wanaponzwa na tabia zao za kuvumilia vitu ambavyo ndani yao havivumiliki.
“Mwanaume akifiwa hali anaugua ndani hata anaweza kukerwa akanyamaza. Kuna kitu kinamsumbua moyo hamwambii mtu atazungumza mambo mengine lakini vitu vya ndani hasemi.
“Tabia ya kutokuongea, kuogopa kudhalilika inasababisha kupata shida. Wanaume wanaamini wanawake ni dhaifu kwa sababu hawawezi kunyamaza, wanahisia lakini hii ndio inasaidia, hawajui kuwa kujiona imara, hatishwi na kitu ni tatizo,” anasema.
Isack Lema, Msaikolojia Tiba kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) anasema wanaume wanapata magonjwa ya akili kwa sababu mtoto wa kiume amesahaulika katika malezi na uwezeshaji ndani ya jamii.
“Malezi ya mabinti yamebadilika kwa kipindi kirefu kumekuwa na kitu cha kumjengea uwezo binti na wanawake lakini ni nani anayewajengea uwezo vijana wa kiume, ni nani anawajengea uwezo wa kuendelea kuyaona ni yapi yanafaa?” Anauliza.
Lema anasema ni muhimu kwa jamii kushtuka katika hili ili kuokoa afya na maisha ya vijana wa kiume huku akishauri wanaume kupunguza makundi rika yanayoweza kuwatumbukiza katika tabia hatarishi ikiwemo dawa za kulevya.
“Ukiangalia kundi kubwa la wanaume wamejiingiza kwenye matumizi ya vilevi kama pombe, bangi na dawa za kulevya na kutokana na kujiingiza kwenye vilevi vinaathiri ule mfumo wa akili uliopo kwenye mwili wa binadamu na kusababisha mchocheo na mwamko wa magonjwa ya akili,” anabainisha.
MILA NA DESTURI ZATAJWA KUWA KIKWAZO
Mila na desturi katika jamii zinatajwa kuwa sababu za wanaume kupata magonjwa ya akili kwa kiasi kikubwa kutokana na jamii kumwona mwanaume kama kiumbe imara ambaye anaweza kukabiliana na changamoto zote kitu ambacho si kweli.
Mzee wa mila kutoka Kijiji cha Negezi, Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Kasimu Kishiwa anasema mila nyingi za Kitanzania zinamtambua mwanaume kama kiongozi wa familia ambaye anabeba changamoto zote.
Anasema si tu familia lakini pia mwanaume ni kiongozi katika jamii anayebeba majukumu mazito hivyo anatakiwa kuwa imara katika maamuzi na kushughulikia changamoto.
“Unajua sasa mambo yamebadilika, changamoto za maisha zimekuwa nyingi hivyo kuna haja sasa ya wanaume kubadilika kwa kuwashirikisha watu wanaowaamini changamoto zao ili wasaidiwe,” anasema Kishiwa.
VIONGOZI WA DINI WASEMA HAYA
Mchungaji mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Richard Hananja anasema jamii imemfanya mwanaume kuwa maalumu hata anapopata matatizo anakaa nayo hatafuti ufumbuzi, kitu ambacho ni hatari kwa afya ya akili.
Anasema changamoto ya akili inatokea mtu anapotarajia kitu fulani na kutokea kitu kingine na kushindwa kupambana nacho.
“Akili haina umaalumu wowote wala haiwezi kuvumilia changamoto ili kusaidiwa, inahitaji kutafutiwa matibabu yake hivyo wanaume wanatakiwa kuzungumza kuhusu magumu yanayowasibu.”
Kuna umuhimu wanaume kukutana na kujadili changamoto zao ili kuzipatia ufumbuzi, jambo litakalosaidia kuepuka matatizo ya akili.
Shehe Othman Ndamo kutoka Shinyanga anasema katika fikra na kukabiliana na changamoto binadamu wote ni sawa, hivyo ni muhimu wanaume kushirikisha changamoto zao.
“Utatuzi wa changamoto ni sehemu kubwa ya kuondoa ugonjwa ikiwa tutaficha maradhi yatatuumbua hivyo ni vyema wanaume kuepukana na mila na desturi za kunyamaza na matatizo watafute suluhu na watu watakaowasaidia ili kuepuka magonjwa ya akili,” anasisitiza Shehe Ndamo.
NAMNA YA KUJISAIDIA
Msaikolojia Bwaya anasema wanaume wakubali kuwa kuna vitu wakivishikilia kama alama ya uanaume vinaweza kuwaponza akiwataka kujenga mifumo itakayowasaidia kutoa sumu kwenye mioyo yao.
“Wawe na watu wa karibu ambao anaweza kuwaambia vitu vyao bila kuogopa atakuona vipi. Kuwa na marafiki wa karibu kama wanawake wanavyofanya kuwa na marafiki na kuongea nao.
“La pili kujenga tabia ya kushughulikia vitu na si kusubiri tatizo kuwa kubwa, mwanaume anapohisi ana maumivu atafute msaada wa wataalamu,” anasema Bwaya.
Bwaya anasema wanaume waoneshe hisia pale wanapojisikia vibaya ikiwemo huzuni na kulia ili kukabiliana na tatizo la ugonjwa wa akili.
“Wanaume tunazungumza kwa namna gani, kuna vile vikao vya kiume, vikao vya baba na kijana wake, kaka na mdogo. Hivi vikao tuzungumze kuelezea hisia zetu na wakati mwingine si tu kuonesha uwezo tulionao lakini pia namna gani tunaweza kupambana na madhaifu yaliyopo.”
Pia wanaume wanashauriwa kutokutumia vilevi kama sehemu mojawapo ya kuendana na maisha bali watafute maarifa ya kutatua changamoto zao.