Sababu zaelezwa watoto wachanga kugeuka njano

TAFITI zimeonesha kuwa tatizo la manjano likitokea ndani ya saa 24 baada ya kuzaliwa mtoto, ni suala la kiafya na kuwa jambo la muhimu ni kutambua sababu na kutoa tiba stahiki.

Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel alisema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Mariam Kisangi (CCM).

Katika swali lake Kisangi, aliuliza iwapo serikali haioni haja ya kufanya utafiti kujua chanzo cha watoto wachanga kugeuka njano baada ya kuzaliwa na mama kuishiwa nguvu.

Dk Mollell alisema tafiti nyingi zimefanyika kitaifa na kimataifa kujua chanzo cha watoto wachanga kugeuka njano baada ya kuzaliwa.

Alisema zimeonesha kuwa hali ya umanjano ikitokea ndani ya saa 24 baada ya kuzaliwa inaonesha tatizo la kiafya na kuwa inatakiwa kutambua sababu na kutoa tiba stahiki.

Dk Mollel alisema tatizo hilo likitokea baada ya saa 24, mara nyingi linatokana na sababu za kawaida za mwili wa mtoto kupunguza chembechembe nyekundu nyingi alizokuwa nazo tumboni kwa mama na kuwa pia uchunguzi wa kina ni muhimu ili kujihakikishia.

“Suala la utafiti ni muhimu na ni suala endelevu katika tiba,” alisema Dk Mollel.

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button