Sababu zatajwa uhaba wa nazi

WAZIRI wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Shamata Shaame Khamis amesema kasi ya ujenzi wa nyumba za makazi na ongezeko la matumizi ya minazi, vimechangia uhaba wa zao hilo Zanzibar.

Shamata alisema hayo wakati akijibu swali la Mwakilishi wa Jimbo la Mwanakwerekwe, Ameir Abdallah Ameir aliyetaka kufahamu sababu za kupungua kwa uzalishaji wa zao la nazi nchini.

Akitoa ufafanuzi zaidi, Khamis alisema kumejitokeza kasi ya ujenzi wa nyumba za makazi katika maeneo mbalimbali ambayo baadhi yake ni yenye rutuba kwa ajili ya kilimo.

Alisema zaidi ya eneo la asilimia 60 ambalo ni lenye rutuba na kustawi kwa zao la nazi hivi sasa limekuwa likiongezeka kasi ya ujenzi wa nyumba za kuishi ambapo wananchi hulazimika kukata minazi kupisha ujenzi.

”Moja ya sababu kubwa za kupungua kwa uzalishaji wa zao la nazi ni ukataji wa minazi kwa ajili ya kupisha ujenzi wa nyumba za kuishi kwa eneo kubwa,” alisema.

Aidha, alisema matumizi ya mbao za minazi yameongezeka katika kutengeneza samani kwa matumizi ya nyumbani ikiwamo vitanda pamoja na viti.

Alisema hivi sasa imebainika hoteli nyingi za kitalii samani zake wanatumia minazi kwa ajili ya kutengeneza vitanda kutokana na mvuto wake na ubora.

”Tumefanya utafiti na tumebaini matumizi ya mbao za mnazi kwa ajili ya kutengeneza samani umeongezeka maradufu ambapo hoteli mpya za kitalii zinategemea mnazi katika kutengeneza vitanda na vitu vingine,” alisema.

Alisema Wizara ya Kilimo imeanza kuchukua hatua mbalimbali kupitia mradi wa kuimarisha zao la minazi kupitia washirika wa maendeleo juu ya njia bora zaidi ya kuimarisha zao hilo.

Alitaja hatua hizo ikiwamo kuotesha zaidi mbegu ya minazi mirefu ambayo ni maarufu katika mwambao wa pwani ya Afrika ya Mashariki kwa kustawi na kudumu kwa muda mrefu.

Aidha, alisema wamejipanga kuotesha zaidi ya miche ya minazi milioni tatu katika kipindi cha miaka miwili huku wakiongeza mbegu za minazi kwa ajili ya madafu.

”Utafiti wetu umebaini kwamba matumizi ya madafu yamekuwa yakiongezeka ambayo ni miongoni mwa sababu za kupungua kwa uzalishaji na upatikanaji wa nazi,” alisema.

Katika miaka ya 1960 Zanzibar ilikuwa ikiongoza Afrika kwa uzalishaji wa nazi pamoja na kusafirisha nje ya nchi ikiwamo bidhaa nyingine za mbata kwa ajili ya uzalishaji wa mafuta.

 

Habari Zifananazo

Back to top button