SACCOS watakiwa kujisajili

MWANZA: VYAMA vya Ushirika wa Akiba na Mikopo Nchini(SACCOS) vimetakiwa kujisajili iliĀ kutambulika kisheria.
Wito huo ulitolewa leo na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Nchini(TCDC) Dk Benson Ndiege wakati wa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya ushirika wa akiba na mikopo(SACCOS) kitaifa iliyofanyika katika viwanja vya Furahisha mkoani Mwanza.
Dk Ndiege amesema katika mwaka huu vyama vya ushirika 1211 viliomba leseni lakini vyama vilivyokidhi vigezo ni vyama vya ushirika 845 ndio vilipata. Amesema vyama 386 havikuwa na vigezo vya kupata leseni.
Amesema vyama vya ushirika vyote nchini vinatakiwa kufanya kazi kwa kutumia leseni zao na wasiofanya hivyo wanakosea.
Amesema katika mwaka 2022 vyama vya ushirika vimeweza kuwa na mtaji wa Sh bilioni 846 na mwaka huu vyama vya ushirika vimeweza kukusanya mtaji wa Sh trilioni 1.2.
Kaimu katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Daniel Machunda amesema katika Mkoa wa Mwanza kuna vyama vya ushirika 371 na vyama hivyo vina wananchama 14000.
Amesema vyama vya ushirika vya Mkoa wa Mwanza kila mwaka vyama hivyo vimekuwa vikitoa mkopo wa Sh bilioni 12.5 na mikopo hiyo ni mikopo ya biashara,Elimu na Kilimo.
Amesema Serikali ya mkoa wa Mwanza itaendelea kuhamasisha Wananchi kujiunga na vyama vya ushirika . Machunda amesema vyama vya ushirika vimesaidia sana katika kuweza kuleta maendeleo katika jamii.