SAA 3 asubuhi ya Juni 6, 2023, tunafika mjini Mwanga. Tunaanza safari kwa gari aina ya Toyota Noah kwenda kijijini Chomvu katika Tarafa ya Usangi, wilayani Mwanga, Mkoa wa Kilimanjaro.
Gari inapanda Milima ya Usangi katika barabara yenye kona zisizohesabika. Hata hivyo, inapanda bila matatizo kutokana na barabara husika kuwa ya lami. Tunashuhudia misitu ya asili iliyopamba milima hiyo.
Tunafika katika Kitongoji cha Kikweni kilichopo Kata ya Msangeni na kukuta njia panda. Zipo barabara kuu mbili; moja ya kwenda Tarafa ya Ugweno na nyingine inakwenda Tarafa ya Usangi. Tunafuata barabara ya kulia inayokwenda Usangi itufikishe kwenye Kijiji cha Chomvu.
Tunapita vijiji kadhaa ikiwa ni pamoja na Sereni Kata ya Msangeni na baadaye Shighatini ambacho kipo Kata ya Usangi. Jina la kijiji hiki linakuwa si geni kutokana na shule kongwe ya Shighatini iliyopo kijijini hapo inayomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mwanga.
Wenyeji wanatueleza kuwa eneo hilo la Shighatini ndio mpaka wa Ugweno na Usangi.
Tunaendelea na safari yetu iliyotuchukua takribani dakika 40 kutoka Mwanga Mjini hadi Kijiji cha Chomvu kilichopo Tarafa ya Usangi.
Katika Kijiji cha Chomvu, tunapokewa na hali ya hewa nzuri ya baridi wastani, yenye ukungu. Hewa ni safi kutokana na miti pamoja na mimea ya kupandwa iliyofunika eneo hilo lenye nyumba bora.
Tunajipatia kifungua kinywa katika mghahawa kijijini hapo. Chapati, maharage na chai vinaongeza nguvu na uchangamfu wa mwili kabla ya kuhitimisha safari kwa mwenyeji mlengwa.
Ashukuriwe mkuu wetu wa msafara, Christopher Majaliwa aliyemudu kugharimia kifungua kinywa hicho kwa watu sita, tukashiba kwa gharama ya Sh 5,600. Ina maana ni wastani wa Sh 900 kwa kila mmoja. Raha iliyoje ya kijijini!
Yumkini, tungekuwa na muda wa kutosha kijijini hapo, tungejipatia vyakula mbalimbali ikiwamo kande ambacho ni chakula kikuu cha wenyeji wa eneo hilo ambao ni mchanganyiko wa Wapare na Wagweno. Vilevile tungepata matunda, hususani maparachichi na mafenesi ambayo tulishuhudia yakiuzwa kwa wingi katika maeneo mbalimbali yaliyochangamka.
Sisahau pia mahindi ya kuchoma ambayo tuliyafaidi katika eneo la Kikweni wakati tukirejea Mwanga Mjini kuelekea Moshi kwa ajili ya safari ya maandalizi ya safari ya kurejea Dar es Salaam ambako ndiko makao makuu ya TSN.
Sikumuuliza mwenzetu, Abduel Elinaza (mwenyeji wa Mwanga) alitumia kiasi gani kuwezesha sote tuliokuwa kwenye Noah kufaidi mahindi hayo.
Yalikuwa ya moto na yenye ladha, yaliyovunwa moja kwa moja kwenye mashamba ya wenyeji wa Mwanga. Kama ingelikuwa Dar es Salaam, mahindi yangetugharimu zaidi ya Sh 5,000 na tungelazimika kuyatia chumvi na pilipili ili kuyapa ladha lakini kwa kijijini hapo, naamini mfadhili wetu alilipa si zaidi ya Sh 3,000.
Haya yote tunayashuhudia kwa sababu ya safari ya kikazi. Hatupati shida ya kufika nyumbani kwa mwenyeji wetu katika Kijiji cha Chomvu kwani anafahamika (sina shaka) kwa kila mwanakijiji.
Baada ya takribani dakika kadhaa za kuvinjari eneo la maduka sambamba na kupata ‘chai’ kwenye mghahawa, wenyeji wanatuelekeza barabara ya kuingia kwa mwenyeji wetu.
Tunaanza kuingia kwenye boma tukishuhudia miti mirefu iliyopandwa kwa mpangilio, hatimaye kuifikia nyumba iliyozungukwa na msitu wenye kuvutia ikiakisi mandhari nzima ya kijiji.
Tunakaribishwa hadi ghorofani ambako tunapata nafasi nzuri ya kufahamu uzuri na umuhimu wa kuhifadhi mazingira! Maana unaona sehemu ya Kijiji cha Chomvu katika ubora wake kimazingira.
“Karibuni sana…Mmepita kwenye milima yetu. Au mmeizoea?” Mwenyeji wetu anatukaribisha. Huyu si mwingine, bali ni Cleopa Msuya. Mwanasiasa mkongwe, Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais mstaafu. Wilayani Mwanga anafahamika kama ‘Baba wa Mwanga’.
Anatupokea kwa ukarimu mkubwa akionesha utayari wa kuzungumza na sisi. Sisi ni akina nani? Ni timu ya waandishi kutoka Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN).
TSN inayochapisha magazeti ya HabariLEO na Daily News, imeandaa programu maalumu ya kuzungumza na viongozi wastaafu na kuyachapisha katika vyombo vyake vya habari kwa maslahi mapana ya taifa.
Miongoni mwa wastaafu ambao wameshahojiwa chini ya mpango huu ni pamoja na mwanasiasa mkongwe na mwanaharakati wa masuala ya jinsia, Balozi Getrude Mongella, Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu, Marten Lumbanga na Spika mstaafu, Pius Msekwa.
Tukiongozwa na Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Habari wa TSN, Christopher Majaliwa, nyumbani kwa Msuya, tunapewa fursa ya kumuuliza maswali mbalimbali ambayo anayajibu na kuyafafanua kwa ufasaha.
Umri wake wa miaka 92 si kikwazo hata kidogo cha kuzungumza kwa ufasaha na kukumbuka mambo mbalimbali hususani tangu alipomaliza Darasa la Nne mwaka 1943 hadi nafasi mbalimbali za juu alizotumikia taifa kabla ya kuamua kustaafu mwaka 2000 akiwa Mbunge wa Mwanga.
Ukiacha mkuu wa msafara, Majaliwa na Abduel Elinaza aliyetuongoza kufika Mwanga kutokana na uenyeji wake, waandishi wengine wa TSN walioshiriki safari hii ya kikazi, Edward Qorro wa Daily News na Ben Shija, ni mashuhuda watakaojuza mengi ya yaliyojiri, ikiwamo undani wa mahojiano yetu na kiongozi huyu mstaafu.
Endelea kufuatilia magazeti yetu ya HabariLEO, Daily News na mitandao yetu wiki ijayo upate kusoma mambo mbalimbali ambayo mengine hukuwahi kuyafahamu kutoka kwa Msuya ambaye baada ya kustaafu, wananchi wilayani Mwanga walimpa hadhi ya kuwa Baba wa Mwanga.