Sagini: Watendaji madawati ya jinsia tunzeni siri

DODOMA: Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanne Sagini, amewataka watendaji wa madawati ya jinsia ndani ya Jeshi la Polisi nchini kujiepusha na tabia za utoaji wa siri za waliopitia vitendo vya ukatili wa kijinsia hali inayosababisha Wananchi kushindwa kutoa taarifa za ukatili.

Naibu Waziri Sagini alisema hayo jijini Dodoma wakati akifungua kikao cha watendaji wa madawati ya jinsia na watoto nchini.

Naibu Waziri Sagini amesema kuwa, kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wateja ambao wamekuwa wakipeleka malalamiko katika Jeshi hilo na kueleza kuwa Askari wanaofanya hivyo ni kwenda kinyume na maadili ya jeshi hilo.

Advertisement

Kwa upande wake Kamishna wa Kamisheni ya Polisi jamii ,CP Faustine Shilogile ameeleza njia mbalimbali ambazo Jeshi hilo linatumia katika kupambana na ukatili wa kijinsia ikiwemo kutoa elimu ya ukatili dhidi ya watoto na wanawake pamoja na kupinga mila potofu.

Naye Mwakilishi Mkazi UN Women Tanzania, Lucy Tesha akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa shirika hilo alisema kuwa UN Women mpaka sasa walishajenga vituo nane vya dawati la jinsia na watoto na wanatarajia kufanya tathimini ya mpango kazi wa kitaifa wa kutokomeza ukatili wa jinsia ambao utaanza mwaka 2024 huku akiahidi kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kutokomeza ukatili wa kijinsia.

Aidha, Mkuu wa Dawati la Jinsia  na Watoto nchini Naibu Kamishna wa Polisi, DCP Maria Nzuki ameeleza changamoto mbalimbali ambazo zinakabili ofisi za dawati la jinsia nchini ikiwemo uchache wa majengo ya uendeshaji dawati hilo, ukosefu wa vyombo vya usafiri ili kuwawezesha kuwafikia waathirikia wa matukio ya ukatili wa kijinsia.

 

 

2 comments

Comments are closed.

/* */