SAIDI NDEE :Kijana aliyepoteza kazi, akaibukia kwenye ubunifu

  • Alifukuzwa kazi, hakukata tamaa
  • Ubunifu wamuuza nchi mbalimbali

KATIKA maisha watu wengi wamejikuta wakikata tamaa hasa baada ya kufukuzwa kazi na kuamini kwamba huenda maisha yakayumba na kupoteza kila kitu cha thamani au hata utu wake.

Lakini kukata tamaa ni jambo baya sana kwa kuwa kila kitu kinakuja kwa sababu maalumu na kwa wakati maalumu, mwanamitindo ambaye anafanya vizuri hivi sasa, Saidi Ndee maarufu kama  Pichichi anasimulia jinsi alivyosota kabla ya kuwa mbunifu wa mitindo.

Akizungumza na HabariLEO Jumapili, Ndee anaelezea zaidi kwa nini aliamua kuingia kwenye ubunifu wa mavazi ya stara baada ya kufukuzwa kazi katika kampuni aliyokuwa akiifanyia kazi.

Anasema baada ya kufukuzwa kazi katika kampuni aliyokuwa akifanyia kazi ambayo hakupenda kuitaja jina, akiwa kama mtaalamu wa masuala ya uhasibu, ilibidi kubaki mtaani kwa ajili ya kujipanga na maisha mapya.

Saidi anaeleza kuwa kipindi hicho aliamua kufanya shughuli ndogo ndogo kujiingizia riziki, lakini hali haikuwa nzuri kiasi cha kujikuta maisha yamekuwa magumu lakini alikataa kukata tamaa.

Kuuza ubunifu

Anasema mwaka 2019 kulikuwa na rafiki yake anayeitwa Maulid anayefanya kazi Kariakoo katika duka lake la Mau Fashion, alikuwa akichukua mzigo China na kuuza Kariakoo.

Saidi anasema kipindi hicho kulikuwa na kilemba maarufu kutoka nchini China, kilikuwa kikitamba sana Kariakoo hivyo Mau alipokutana na rafiki yake huyo (Ndee) alimpa kazi ya kutafuta fundi ili aweze kukishona hapa hapa nchini.

“Mau alikuwa kama mtu ambaye aliamua kunisaidia kwa kunipa kazi ili nisibaki kuwa nyuma, maana alikuwa ananijua hali ambayo nilikuwa naipitia,” anasema.

Kwa mujibu wa Ndee, kwa kuwa alikuwa na uelewa kidogo wa masuala ya ubunifu, ilibidi kuuchora tena ule mchoro mtandio ili ampelekee fundi na aweze kuushona.

Anasema alihangaika na michoro kadhaa ili kupata ulio bora, ndipo akafanikiwa kuupata mchoro wa kofia aliyoletewa sasa ikawa kazi kumpata fundi ambaye ataweza kushona kama ambavyo inatakiwa kuwa.

“Kuna mtu alinielekeza kwamba ninaweza kupata mafundi wazuri pale Machinga Complex, ilibidi niende, nikapata baadhi ya mafundi na kuwapa maelekezo vile ambavyo nahitaji iwe,” anasema.

Saidi anasema kupata kilemba cha kwanza na kukitumia kama mfano kwa Mau, alimruhusu akashone dazeni 20 za vilemba hivyo na vilemba 50 kwa ajili ya soko la Kariakoo.

Vazi la stara,moja katka kazi za ubunifu wake.

Anasema alifanikiwa kushona vitambaa hivyo na kumpelekea na kwa mara ya kwanza anaanza kupata mwangaza katika macho yake baada ya kuambiwa kilemba kile kimeuzika vizuri sokoni na kiliisha chote.

Kufanya vizuri kwa kilemba cha kwanza, ndipo alipopata wazo la kubuni kilemba cha pili ili kujitafutia ajira yake binafsi kupitia sanaa hiyo ya ubunifu.

Anasema ilibidi kujifungia ndani mwenyewe, akabuni kilemba kofia kingine alichokipa jina ‘mwendokasi’ ambapo hii aliongeza mauzo na kumfanya rafiki yake afurahie uwepo wake katika biashara hiyo.

Kujiingiza katika biashara rasmi

Mwaka 2020 aliamua kijiingiza katika biashara rasmi baada ya kuona inamlipa kwa kuanza kufungua mtandao wa kijamii kwa jina la PichichiTurbans, huko akaanza kusambaza vilemba vyake na kufanya watu wengi waanze kuvutiwa naye.

Anasema kupitia mitandao ya kijamii alianza kupata wateja mbalimbali, lakini changamoto ikawa wateja wapotaka kupafahamu ofisini kwake wakati hakuwa na ofisi.

“Watu wengi walikuwa wakijua Pichichi ni mwanamke, watu wakawa wananiuliza dada tunakupata wapi. Jambo hilo lilikuwa linanifanya mpaka nashindwa kujitokeza mimi kama mimi,” anasema.

Anasema Julai 2020 alienda kupeleka bidhaa zake kwenye maonesho ya biashara ya kimataifa maarufu kama Sabasaba yaliyokuwa yakifanyika mkoani Dar es Salaam na ndipo akapata mwangaza mkubwa baada ya watu kuzidi kutamani kujua ofisi yake ilikuwa wapi.

Baadhi ya dizaini mpya zipatikanazo katika duka la Pichichi,Kariakoo.

Kwa mujibu wa Ndee, alimpa dada mmoja aliyejulikana kama Christina, raia wa Kenya bidhaa zake na dada huyo akamfundisha jinsi ya kutanua biashara yake kwa njia nyingine zaidi.

Anasema alianza kushona vilemba kofia vya aina tofauti tofauti na kupita Kariakoo kwa watu wenye meza na kuzisambaza ili wauze.

Kofia zinazobaki alikuwa akizipitia jioni na faida inayopatikana wakawa wanagawana na hapo akatengeneza mtandao mkubwa wa wafanyabiashara wadogo wenye meza kwa ajili ya kumuuzia biadhaa zake hizo.

“Sasa kitu cha msingi kilikuwa ni wapi kupata ofisi, maana Kariakoo gharama ilikuwa kubwa sana. Hivyo ikabidi nipambane sana,” anasema.

Abuni vazi la stara na heshima

Anasema mwaka 2021 alipata fremu maeneo ya Kariakoo karibu na Hoteli ya Wanyama na aliamua kununua cherehani mbili, kwa hiyo upande mmoja aliweka cherehani kwa ajili ya kushona na upande wa pili akaigeuza eneo la kuuzia kofia zake.

Saidi anasema duka hilo likawa ndiyo sehemu yake na wateja wake wote akawa anawaonesha, hata wafanyabiashara wadogo wadogo wakawa wanamfuata na siyo tena kuwapelekea mizigo.

Anasema tayari akili yake ikazama ni jinsi gani anaweza kutengeneza fedha zaidi, aliamini biashara ya kofia inaenda ipo siku itabadilika na huenda soko likapotea kabisa.

Dizaini za Kofia

Anaongeza kuwa akafikiria kubuni vazi ambalo litaendana na kofia hizo, kwa kuwa hata wateja wake nao walipokuwa wakiagiza kofia kupitia mtandaoni walikuwa wakiuliza na mavazi watayapata wapi.

Saidi anasema kama ilivyokuwa kwa kofia aliweza kupambana na kubuni vazi lake la kwanza, ambalo aliliita jina la ‘hijabu ya kisasa’ ambalo aliliingiza sokoni mwaka 2021 na lilifanya vizuri zaidi.

Baada ya hapo akaanza kutengeneza mavazi mbalimbali na alijifunza kupitia uvaaji wa Rais Samia Suluhu Hassan.

“Rais alikuwa kama kioo kwangu, nikapata mawazo mengi na kujua naweza kubuni vazi gani la stara na heshima kupitia mavazi yake,” anasema.

Kwa mara ya kwanza wakati anaingia madarakani, Ndee anasema aliweza kubuni vazi lililoitwa Koti la Samia, ambalo lilitokana na nguo zake za kitenge na koti na  lilifanya vizuri sana.

Koti la mama Samia lilikwenda mbali zaidi na watu wakawa wanauza hadi katika nchi za jirani, ikiwemo Comoro, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na nchi zingine za jirani, ambapo vazi hilo lilipokelewa vizuri.

Saidi anasema kupitia vazi alilovaa Rais Samia katika filamu ya Royal Tour aliweza kubuni na kutengeneza vazi la Royal Tour ambalo lilikuwa ni viatu, kombati na kofia.

“Vazi la Mama Samia Tour lilishinda tuzo mbalimbali, ikiwemo hapa nchini na nchini Zambia… hili vazi lilikuwa maalumu kwa ajili ya kutangaza utalii wa ndani, na katika kila onesho watu wengi walikuwa wakiniuliza kwa nini nililiita jina hilo ndipo nilipokuwa napata nafasi ya kuitangaza nchi yangu kwa kuelezea,” anasema.

Anasema akaanza kutengeneza mavazi kulingana na wakati na kuwa alitengeneza mavazi mbalimbali kama mavazi ya Corona alililotengeneza kipindi cha Covid-19 imepamba moto na kufunga vitakasa mikono, lakini alitengeneza kofia za Fly Over na mavazi mengine ambapo yalimpa jina ndani na nje ya nchi ikiwemo vazi la Mayotte lililopata jina la kisiwa cha Mayotte  kilichopo Bahari ya Hindi kati ya nchi ya Comoro na Msumbiji.

Tuzo alizozipata

Saidi au maarufu kama Pichichi, anasema mwaka 2000 alisikia shindano la mavazi lililokuwa limeandaliwa na kampuni ya Stara Fashion Show lililokuwa likishindanisha mavazi ya heshima na star, ingawa aliogopa  kwenda kupeleka mavazi yake.

“Kitu ambacho kilikuwa kikiniogopesha zaidi ni kwamba watu ambao walikuwa wakiwasiliana na mimi na kununua mavazi yangu, walikuwa wakijua kwamba Pichichi ni mwanamke na ingekuwaje nikijitokeza mimi,” anasema.

Saidi anasema ilibidi kughairi kwenda kwenye maonesho hayo, lakini rafiki yake wa karibu na mtu ambaye wanashirikiana katika masuala ya kazi alimwambia ni bora kujitokeza kuliko kukaa kimya na baadaye kujitokeza mtu na kujitambulisha jina hilo.

Baada ya  hapo anasema alipata ujasiri na kwenda kuomba fomu ya kujiunga, ingawa aliambiwa tayari muda ulikuwa umeshapita na mashindano yalikuwa tayari kuanza.

Anasema hata hivyo baada ya kuona nguo zake walikubaliana naye na kumpa nafasi ya kuonesha mavazi yake kwa mara ya kwanza na alipeleka mavazi ah ap tofauti.

Katika shindano hilo anasema hakushinda ila ulikuwa mwanzo hapo kuungwa katika kampuni iliyoandaa mashindano hayo na kila walipokuwa wakienda kufanya matamasha alichukuliwa kupeleka nguo zake.

Anabainisha kuwa baada ya ah apo akaanza kushinda tuzo mbalimbali, ikiwemo tuzo moja aliyoshinda nchini Zambia kupitia vazi la Royal Tour, akashinda tuzo nyingine kupitia vazi la heshima lililochanganywa na batiki.

Moja ya tuzo aliyoshinda nchini Malawi.

Baada ah apo akaanza kushinda tuzo na kupewa vyeti mbalimbali, ambavyo vingine vilitokana na kwenda kujiongezea ujuzi kidogo katika elimu ya ubunifu katika vyuo mbalimbali.

Kutokana na kujitangaza kwake alianza kupata nafasi ya kushiriki mikutano mbalimbali na kuwavisha watu maarufu akiwemo muigizaji Zuhura Othman Soud  ‘Zuchu’ kwa kubuni vazi la Ramadhani, mfanyabiashara na msanii, Zuwena ‘Shilole’  na waigizaji wengine.

Lakini pia alipata nafasi ya kuwavalisha viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Pangani, Zainabu Abdallah, lakini pia kuvalisha wanawake mawakili katika mkutano wao uliofanyika Tanga.

Maisha yake

Mbunifu huyu anasema jina Pichichi linajulikana zaidi Karikaoo na kwenye mitandao ya kijamii hasa katika tasnia ya ubunifu wa mavazi, lakini upande wa wazazi wake anajulikana kama Saidi Ndee, mzaliwa wa Mkoa wa Dodoma.

Saidi ni mtoto wa nne katika familia ya watu 10 ya Hassan Ndee. Alifanikiwa kupata elimu yake ya msingi katika Shule ya Msingi Chamwino, baada ya hapo akajiunga na Shule ya Sekondari Dodoma Mjini na alihitimu kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari Ubwe.

Baada ya kumaliza elimu ya sekondari alijiunga katika Chuo cha Biashara (CBE) na kuchukua masomo ya uhasibu, baada ya hapo alipata kazi kama mhasibu katika moja ya ofisi mkoani Dar es Salaam.

Anasema amepata mafanikio makubwa kupitia kazi ya ubunifu na ushonaji, ubunifu umemuwezesha kujuana na viongozi mbalimbali na kuwa na nafasi ya kutembelea nchi tofauti.

Saidi anasema pia amepata nafasi ya kuendesha familia yake na kutoa ajira kwa vijana wenzake, kwa kuwa amefungua duka kubwa zaidi na kuajiri mafundi na wengine wakifanya kazi kama vibarua.

Lakini anasema pia amekuwa akifanya biashara na wakazi wa nchi tofauti kwa kuwa wanafika dukani kwake na kuagiza mzigo ambao umekuwa ukienda katika nchi zao.

Hata hivyo, anasema kumekuwa na changamoto mbalimbali, lakini  mojawapo ni kuwa anaweza kubuni vazi na kabla halijaingia sokoni au baada ya muda mfupi kuingia sokoni, anakuta limeletwa na Mtazania mwingine aliyekwenda kulitengeneza China.

Mbunifu Said Ndee na Modo wa kazi zake.

Habari Zifananazo

Back to top button