Saitoti, wenzake 7 kortini Simanjiro

MFANYABIASHARA maarufu wa madini ya tanzanite Jiji la Arusha, Joel Mollel maarufu kwa jina la Saitoti, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Gem & Rock Venture na wenzake saba leo wamepandishwa kizimbani Mahakama ya Wilaya ya Simanjiro, mkoani Manyara kujibu mashtaka mawili ya shambulio na kukaidi amri ya Wizara ya Madini Machi 13, 2023 Mgodi wa Kitalu C unaomilikiwa na serikali na mwekezaji mzawa Onesmo Mbise.

Mbali ya Saitoti washitakiwa wengine ni Petro Exsaud (48) mkazi wa Moshono Arusha, Mosses Kelerwa(45) mkazi wa Mirerani, Daniel Siyaya(44) mkazi wa Ilboru Arusha, Mosses Sirikwa (46) mkazi wa Ilboru, Dausen Mollel(58) mkazi wa Ilboru na Enock Nanyaro(32) mkazi wa Arusha.

Wakisomewa mashitaka na Mwendesha Mashitka wa Polisi, Mosses Hamilton mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Simanjiro, Charles Uiso, ilidaiwa kuwa katika shitaka la kwanza linalowahusu wote saba kwamba waliwashambulia kwa majabali na silaha za uchimbaji wafanyakazi sita wa Kampuni Franone inayochimba mgodi wa madini ya tanzanite Kitalu C kwa kushirikiana na serikali.

Shitaka la pili linawahusu washitakiwa wawili Saitoti na Enock Mollel, ambao ilidaiwa wameshitakiwa kwa kwa shitaka moja la kukaidi amri ya Wizara ya Madini, ambapo ilidaiwa kuwa walizuiwa kufanya shughuli za uchimbaji katika eneo hilo. Washitakiwa wote walikana shitakana hilo na walikidhi vigezo vya dhamana, kesi hiyo itatajwa tena Aprill 14 mwaka huu.

 

Habari Zifananazo

Back to top button