MWANARIADHA Jackline Sakilu wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), amechaguliwa kuwa Mwanamichezo Bora wa Tanzania kwa mwezi Februari, 2024 katika tuzo zinazotolewa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo nchini (TASWA).
Taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Tuzo za TASWA, JemedariSaid, imesema kikao cha kamati hiyo kilichofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam, kilimchagua Sakilu kushinda tuzo hiyo baada ya kung’ara katika mbio za kimataifa za Ras Al Khaimah (RAK Half Marathon), zilizofanyika Dubai Falme za Kiarabu, Februari 24, mwaka huu.
“Katika mbio hizo zinazotambuliwa na Shirikisho la Riadha la Kimataifa (WA), zikiwa na hadhi ya Dhahabu ‘Gold Label’, Sakilu alishika nafasi tatu na kutwaa Medali ya Shaba akitumia saa 1:06.05. Kwa muda huo, Sakilu aliweka rekodi mpya ya Taifa ya mbio za Nusu Marathon, akivunja ile ya saa 1:06.37 iliyokuwa ikishikiliwa na Koplo Magdalena Shauri wa JWTZ.
“Sakilu aliingia fainali ya tuzo hizo na kuwashinda wanamichezo wengine wawili ambao pia walifanya vizuri katika michezo yao kwa mwezi Februari, ambao ni mcheza gofu Isihaka Daud na kiungo mahiri wa mpira wa miguu anayechezea Yanga ya Dar es Salaam, Mudathiri Yahya. TASWA itatangaza siku ya kumpatia tuzo yake mwanariadha huyo,”imesema taarifa hiyo.
Mwanariadha huyo anakuwa mwanamichezo wa pili kutwaa tuzo hiyo mwaka huu, akimfuatia bondia Hassan Mwakinyo aliyefungua dimba kwa kushinda tuzo ya mwezi Januari baada ya TASWA kurejesha tuzo za mwezi na kuzinduliwa Februari 10, 2024 na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ambaye aliwakilishwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye.