Salamu za Rais Samia 2023-2024

IKULU: RAIS Samia Suluhu Hassan amesema 2024 ni mwaka wa utekelezaji na matokeo, hivyo wananchi hawanabudi kubadilika na kufanya kazi kwa bidii, maarifa na uadilifu.

Amesema Serikali itaendelea kusimamia haki, uadilifu, uwajibikaji na nidhamu ya utendaji serikalini.

Ameyasema hayo katika salamu zake za kuuaga mwaka 2023 na kuukaribisha mwaka mpya wa 2024 na kuahidi kuwa Serikali itaendeleza ushirikiano na kampuni changa ili kuzikuza.

“Namuomba Mwenyezi Mungu atujalie kheri na fanaka katika mwaka mpya 2024, uwe ni mwaka wa mafanikio zaidi na tuendelee kufanya kazi kwa weledi, bidii, maarifa na uadilifu ili kazi iendelee,” amesema Rais Samia.

Rais amewataka Watanzania kushiriki, kuongeza tija na kupunguza gharama za uzalishaji kwa wakulima na kuhakikisha usalama wa chakula.

Aidha, ameeleza azma ya Serikali kuendeleza  programu ya Jenga Kesho iliyo Bora (BBT), kutekeleza miradi ya kuuza na kukodisha kwa bei ya ruzuku zana za kilimo kwa wakulima ikiwamo matrekta, kuendelea kufanya mageuzi katika sekta mbalimbali ikiwemo uendeshaji wa mashirika ya umma na taasisi ili kuongeza ufanisi na tija katika uendeshaji wake.

Amesema mwaka 2024 kutakuwa na maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano na miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ambayo ni muhimu katika kudumisha umoja wa kitaifa.

Rais hakusita pia kugusia uchaguzi wa Serikali za Mitaa na kusema kutakuwa na uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

Habari Zifananazo

Back to top button