Salma Kikwete asisitiza uvumilivu kwa wana ndoa

MAMA Salma Kikwete, ambaye ni mke wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dk Jakaya Kikwete, amewashauri wanandoa kuishi kwa kuvumiliana, ili waweze kulinda na kudumu katika ndoa zao.

Mama Salma ameyasema hayo leo Ijumaa, wakati akihojiwa na Clouds Media kwenye kipindi cha Leo Tena na kusema msingi mzuri wa kuimarisha ndoa na familia ni uvumilivu baina ya wanandoa.

“Vikombe vikikaa pamoja lazima vitagongana, haviachani kugongana, lazima vitagongana, lakini kikubwa ni kuvumiliana. Mimi namvumilia na yeye sio kwamba mimi sina mapungufu, ananivumilia. Ana uwezo mkubwa wa kunivumilia,” alisema Mama Salma.

Amewashauri wanandoa kuishi kwa kuaminiana, huku akisema chanzo kikubwa cha kuvurugika kwa ndoa ni matumizi ya simu yanayosababishwa na kukosekana kwa imani baina ya wana ndoa.

“Kitu ambacho sasa hivi kinaharibu mahusiano watu wanafikia kutoaminiana ni simu, kwa mfano kama hapa hivi mimi nina simu yangu, simu ile ikiita kabla mwenyewe hajaipokea umeipokea wewe na kuanza kuiperuzi na yeye kuiperuzi ya kwako, hapo hutokea migongano hasa inapotokea kwamba kuna vitu huko nyuma.

“Ila mimi simu yangu naiweka kokote, watoto wangu wanaiangalia, wanapokea na hata mume wangu anapokea simu yangu suala kubwa ni kuaminiana na kujua ninyi ndio wana ndoa,” alisema Salma Kikwete.

Kwa upande wake Rais Mstaafu, Jakaya Mrisho Kikwete amesema msingi mwingine mzuri wa kuimarisha na kupunguza matatizo ya kuvunjika kwa ndoa ni kutokuruhusu tofauti kukaa muda mrefu.

“Sisi tuna miaka zaidi ya 30 sasa, haiwezekani we hakuna siku mkatofautiana. Sasa ni jinsi gani mnakabili zile tofauti.

“Kuna siku anakasirika sana huyu (Mama Salma) na akikasirika sana mi nanyamaza, lakini sasa akipandisha nami nikapandisha hapo ndo mnakwenda mnafika mahali mnaharibikiwa kabisa,” alisema.

Habari Zifananazo

Back to top button