Salva Kiir ataka wananchi kuchangamkia kilimo

Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir

RAIS Salva Kiir amewataka wananchi kushiriki kikamilifu katika kilimo kwa sababu ndio kazi pekee itakayosaidia kuimarisha maisha yao na kuleta ustawi wa jamii.

Kwa sasa dunia ikikabiliwa na changamoto kubwa ya kupanda kwa gharama za maisha kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo za mabadiliko ya tabianchi na migogoro ya kivita miongoni mwa mataifa kadhaa.

Alisema hayo alipofanya ziara katika shamba lake lililopo katika mkoa alikozaliwa wa Luri Payam Magharibi mwa Mji Mkuu, Juba.

Advertisement

Kwa mujibu wa Rais Kiir, kilimo ni silaha kubwa inayowezesha jamii kushinda vita dhidi ya umasikini na utegemezi kwa nchi.

Katika mazungumzo na vyombo vya habari, Kiir alisema wananchi waliosikiliza ushauri wake kipindi kilichopita sasa wamebadilika kimaisha ikilinganishwa na wale wanaofanya mambo kwa kufuata watakavyo.

“Kama wote tutaamua kuifanya kazi hii kwa nia na moyo mmoja, tutaongeza uzalishaji katika taifa hili kwa kiasi kikubwa hali itakayosababisha kilio cha njaa kumalizika rasmi. Unaweza kulima eneo dogo pembeni ya makazi yako kama unavyoona nyuma yangu,” alisema akionesha shamba la mpunga.

Aliongeza kuwa wananchi wa taifa hilo wanatakiwa kutumia baraka za Mungu kwa taifa hilo kama mito na maziwa kulima mazao kama mpunga unaohitaji maeneo oevu yenye maji na unyevunyevu.

Kauli ya Rais Kiir kwa kiasi kikubwa, iliwaamsha wakulima walioanza kulalamika kuhusu changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya kilimo hususani katika Jimbo la Upper Nile kama vile wadudu waharibifu na ukosefu wa soko la uhakika.