MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania anayechezea klabu ya Genk ya Ubelgiji, Mbwana Samatta amechaguliwa kuwa miongoni mwa wachezaji bora 11 wa muongo mmoja. Mtandao wa Shirikisho la Soka Afrika (Caf) uliweka majina ya wachezaji waliofanya vizuri kuanzia mwaka 2010 hadi 2020.
Kwa mujibu wa mtandao huo, kikosi hicho kimechaguliwa baada ya kura zilizopigwa na mashabiki.
“Hiki ndio kikosi bora cha muongo mmoja, Ligi ya Mabingwa Afrika, kimetokana na kura zenu,” ulisema ujumbe mfupi kwenye mtandao wa Caf wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Samatta alifanya vizuri kwenye michuano hiyo akiwa na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kuanzia mwaka 2011 hadi 2016 na kuisaidia timu hiyo kutwaa ubingwa wa Afrika mwaka 2014/2015.
Msimu huo ndiko ambako nyota ya Samatta iling’ara zaidi baada ya kuibuka mfungaji bora lakini pia mchezaji bora wa Afrika wa CAF kwa wachezaji wa ndani.
Pia, alitajwa kwenye kikosi bora cha mwaka fursa iliyomfungulia milango ya yeye kwenda kucheza soka la kulipwa Ulaya. Wachezaji wengine waliotajwa kwenye orodha ya kikosi bora cha Afrika cha muongo ni mlinda lango kutoka Uganda, Denis Onyango (Mamelodi Sundown’s), Wael Gomma, Ahmed Fatty, Hossam Ghaly, Hossam Ashour, Ali Maaloul na Walid Soliman (Al Ahly-Misri).
Wengine ni mshambuliaji kutoka Zambia, Stopilla Sunzu (TP Mazembe), Percy Tau (Mamelodi Sundown’s na Al Ahly) pamoja na kiungo mshambuliaji kutoka nchini Zimbabwe, Khama Billiat (Kaizer Chief).