Samia aagiza usalama uimarishwe

RAIS Samia Suluhu Hassan, ameliagiza Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kujifunza mbinu mpya za kiulinzi na kiusalama ili kuendana na kasi ya mabadiliko duniani.

Alitoa agizo hilo Alhamis Dar es Salaam kwenye maadhimisho ya miaka 10 tangu kuanzishwa kwa Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC).

Katika maadhimisho hayo, Rais Samia alipewa Tuzo ya Heshima ya NDC kwa kuwa kielelezo cha mwanastratejia mzuri.

Wengine waliopewa tuzo ni Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dk Jakaya Kikwete, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, Rais Mstaafu marehemu Dk John Magufuli na Balozi Mstaafu, Ombeni Sefue.

Rais Samia alisema dunia inabadilika hivyo ni lazima nchi iwe na watu wanaoweza kuisoma na kutabiri yatakayotokea.

“Tumefungua nchi watalii wanaingia wengi, nani anaingia kama mtalii na nani anaingia kivingine, nani anachunguza hayo, tunahitaji wengi, kufunguka kwa nchi kusihatarishe nchi yetu, kuna haja ya kufanya zaidi ya hapa tulipo kwenye masuala ya usalama na ulinzi,” alisema.

Rais Samia alisema serikali kupitia Sera ya Diplomasia ya Uchumi imeifungua nchi hivyo ni vyema nchi ikawa na watu wenye uwezo wa kuusoma mwenendo wa kuifungua nchi na mambo yanayoingia nchini.

Aidha, alisema ipo haja ya kufundisha viongozi na maofisa wengi zaidi katika chuo hicho na kuwapa nafasi zaidi vijana kwa sababu wana nafasi ya kutumikia nchi kwa muda mrefu.

Rais Samia pia aliagiza chuo hicho kitoe kipaumbele kwa wanawake kwa kuwa wana uwezo. “Ongezeni nafasi za masomo kwao sio kwa sababu Rais ni mwanamke, la hasha, bali kwa sababu ni wajenzi na walinzi wazuri wa taifa,” alisema.

Rais Samia alitaka chuo hicho kwenda kufundisha viongozi wa ngazi za chini za serikali katika mikoa na wilaya kwa zababu ndio wanaishi na wananchi kwa ukaribu zaidi hivyo mafunzo hayo yakishushwa kwao yatawajenga ili kuwa na taifa la wazalendo.

“Serikali inajielekeza kukuza uchumi wa wananchi wa chini na hii ni kwa sababu tumeshafanya kwa kiasi juu sasa tunajielekeza kwa wananchi, hivyo kuna haja ya kuwapa mafunzo viongozi walio karibu na wananchi ili wawe na ujuzi na nchi isonge mbele, nitashukuru kama mafunzo hayo yataanza mapema,” alisema Rais Samia.

Akizungumzia sera ya R 4, Rais Samia alisema serikali imefungua nchi kwa sera hiyo ambayo ni upatanishi, kuvumiliana, kuishi pamoja na kuijenga nchi na kusema lengo la serikali ni kutaka kila mtu azielewe hizo R 4 ili wote waende pamoja katika ujenzi wa taifa.

“Naomba chuo kifundishe hiyo sera, ili kulinda usalama na kuwa na maendeleo, biashara inakua nchi imefunguka, tuimarishe usalama wetu wa vinavyoingia, kuna masuala ya vita ya uchumi, vita ya biashara na vita ya mtandao,” alisema Rais Samia.

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Stargomena Tax alimshukuru Rais Samia kwa kukipa chuo hicho Sh bilioni 7.8 katika mwaka wa fedha 2022/23 kwa ajili ya ujenzi wa bweni.

Dk Tax alisema NDC inasaidia kutoa mafunzo ya usalama wa taifa ambao ni jambo muhimu kwa Watanzania wote.

Awali, Mkuu wa Chuo hicho, Michael Mhona alisema wahitimu 1,026 wa kozi ndefu na fupi wamepata mafunzo chuoni hapo tangu kuanzishwa kwake Septemba mwaka 2012.

 

Habari Zifananazo

Back to top button