RAIS Samia Suluhu Hassan ameweka historia mkoani Kigoma kwa kuzima majenereta yaliyokuwa yakitumia Sh bilioni 52 kufua umeme huku mapato yatokanayo na umeme huo yakiwa Sh bilioni 14 pekee kwa mwaka.
Rais Samia alifanya kazi hiyo jana wilayani Kasulu akizima majenereta hayo na kuwasha umeme wa Gridi ya Taifa ambao sasa unawahakikishia wakazi wa mkoa huo wa Magharibi mwa Tanzania umeme wa uhakika.
Alisema majenereta hayo yalikuwa yakitumia Sh milioni 36 za mafuta kwa siku ili kufua umeme na kuusambaza Kasulu na sasa Kigoma imefunguka, na ni miongoni mwa mikoa ya kimkakati katika biashara na uwekezaji.
Alisema wananchi sasa wamepata umeme wa kutosha utakaowasaidia kufanya shughuli zao za kimaendeleo na kuwataka wachangamkie biashara na fursa za uwekezaji.
Rais Samia amewataka wananchi wa Kasulu walinde majenereta hayo na akasema kituo hicho chenye majenereta kitabaki na kulindwa.
“Ombi langu kwenu, pamoja na kuyazima majenereta tunayaweka akiba, naomba sana ni mali yenu yanatunzwa na Tanesco (Shirika la Umeme Tanzania) yalindeni yasiharibiwe, kituo hiki kibaki kama kilivyo mambo ya umeme ni mashine, zikiharibika huko, tunawasha hapa,” alisema Rais Samia.
Alisema Kigoma ni mkoa wa pembezoni mwa nchi hivyo kupeleka umeme wa uhakika ni kuvutia wawekezaji waende kwa wingi kuwekeza.
Awali akizungumzia kuwashwa kwa umeme wa Gridi ya Taifa, Waziri wa Nishati, January Makamba alisema utasaidia kuondoa gharama nyingi za uendeshaji, matengenezo na mafuta.
“Kufika kwa umeme wa gridi Kigoma kuna manufaa mengi ya kiuchumi kwa vituo vyetu hivi vya kuzalisha umeme kwa majenereta ulizalishwa megawati 14, lakini huu wa gridi sasa ni megawati 20,” alisema January.
Katika hatua nyingine, Rais Samia amefungua Barabara ya Kidahwe-Kasulu yenye urefu wa kilometa 63 na aliweka jiwe la msingi la barabara ya Kabingo-Kasulu-Manyovu yenye urefu wa kilometa 260.6.
Aliwataka wananchi waitunze barabara hiyo.
“Tuzitumie vizuri barabara hizi, madereva mwendo kasi unaua, tuache kupaki magari pembezoni na kumwaga mafuta, lindeni barabara zenu, barabara nyingi zinaharibika kabla ya muda wake, niombe sana tutunze barabara zetu,” alisema Rais Samia.
Alisema iwapo Watanzania watatunza barabara serikali itaokoa fedha zinazotengwa kwa matengenezo na zitapelekwa kutekeleza miradi mingine ya maendeleo.
Awali, Rais Samia alizindua Chuo cha Ualimu cha Kanda cha Kabanga chenye uwezo wa kudahili wanafunzi 800, na chenye mabweni ya kubeba wanafunzi 400 kwa wakati mmoja.
Chuo hicho kimejengwa kwa ushirikiano na Serikali ya Canada iliyotoa Dola za Marekani milioni 120 kusaidia sekta ya elimu nchini na pia wanaboresha vyuo vya ualimu vya serikali 35.
Rais Samia alisema lengo la serikali ni kuboresha sekta ya elimu kwa kujenga vyuo vya ualimu vitakavyotoa wataalamu katika sekta ya elimu ili kwenda kufundisha wanafunzi katika shule mbalimbali nchini.
Katika hatua nyingine, Rais Samia amesikia changamoto ya wananchi wa Kigoma kuhusu mawakala wachache wa mbolea na kutopata namba za usajili wa wakulima.
“Waziri wa Kilimo yuko njiani anakuja, ndani ya wiki mbili changamoto zote hizi zitatatuliwa, tutaongeza idadi ya mawakala wa mbolea, tunawashukuru wakulima kwa kujisajili, kuhusu namba za usajili mtandao unasumbua, ila changamoto zote zinashughulikiwa,” alisema.
Pia ameishukuru Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa kuziunganisha nchi za Afrika Mashariki katika mtandao wa barabara na huduma nyingine na kusema wiki ijayo kuna uwekaji wa jiwe la msingi katika ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Msalato mkoani Dodoma ambao pia benki hiyo inaufadhili.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa alisema AfDB pia ni wafadhili wa sehemu ya ujenzi wa barabara ya Nyakanazi-Kabungo hadi Manyovu na kuwa katika kuifungua Kigoma ambayo iko katika ushorobo wa kati, utaunganisha barabara za kwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) na Mbunge wa Kasulu Mjini, Profesa Joyce Ndalichako aliomba serikali kutatua changamoto ya maji, barabara, umeme na upatikanaji wa mbolea jimboni kwake.
“Kwenye barabara niombe sana pamoja na shukrani ninazozitoa, lakini kwenye kazi ya barabara bado sana. Ukienda kwenye Kata ya Muhunga wakati wa mvua hakupitiki kabisa, tuombe suala la barabara katika Mji wa Kasulu lipewe kipaumbele,” alisema Profesa Ndalichako.