RAIS Samia Suluhu Hassan amesema uchumi wa buluu ni fursa na kuwataka wananchi kujipanga na kuweka mazingira mwafaka ya uwekezaji ili waweze kunufaika kupitia rasilimali zinazopatikana katika sekta hiyo.
Alisema hayo katika sherehe za Msimu wa Pili wa Tamasha la Vyakula vya Baharini lililofanyika katika ufukwe wa Kendwa, Mkoa wa Kaskazini Unguja, Zanzibar.
Wakati akisoma hotuba kwa niaba ya Rais, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega alisema maana halisi ya uchumi wa buluu ni matumizi endelevu ya rasilimali zilizomo kwenye bahari, maziwa na mito kwa maendeleo ya uchumi wa Taifa, kutengeneza ajira na kuleta ustawi wa maisha ya watu na vilevile kutunza afya ya maumbile ya bahari.
Rais Samia alisema kupitia tamasha hilo ni muhimu kujizatiti na kujipanga vyema ili kuzitumia vyema fursa zilizopo na zinazojitokeza katika sekta ya uchumi wa buluu.
Aliongeza kwa kusema kuwa ili fursa hizo ziweze kuwa endelevu ni muhimu kuhakikisha kunakuwa na mipango ya matumizi sahihi ya bahari, usimamizi bora wa ikolojia za bahari, kudhibiti uchafuzi wa bahari, kuimarisha uvuvi wa bahari kuu na kusimamia mnyororo wa thamani wa mazao ya baharini na kuimarisha mifumo ya kitaasisi ya usimamizi bora wa uchumi wa buluu na rasilimali zake.
Alieleza kuwa ni muhimu kuweka kipaumbele kwenye hifadhi ya mazingira ya bahari kwani bila kufanya hivyo hakutakuwa na upatikanaji endelevu wa samaki na mazao mengine ya bahari.
“Hili sio suala la Kitaifa tu, bali la Kikanda na Kimataifa, kama mnavyofahamu pamoja na kwamba mabadiliko ya tabianchi yanaathiri maeneo yote ya nchi, maeneo ya visiwa yapo hatarini zaidi. Hivyo, hatuna budi kulisimamia vyema suala la uhifadhi wa mazingira,” alifafanua Rais Samia.
Alibainisha kuwa mipango ya maendeleo ya Kitaifa imeagiza kutekeleza ajenda ya uchumi wa buluu ya Tanzania, kama ilivyoainishwa kwenye Mpango wa (Vision) 2050 kwa Zanzibar na Dira ya Maendeleo ya 2025 kwa Tanzania.
“Pamoja na maelekezo hayo, Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM 20/20 inatuelekeza kuongeza uzalishaji wa samaki na mazao ya baharini, ujenzi wa miundombinu ya uchumi, ujenzi wa masoko ya kisasa na viwanda vya usindikaji wa samaki na ununuzi wa meli za uvuvi,” alisema.
Rais Samia alisema kuwa kufuatia fursa zilizopo katika uchumi wa buluu ambazo zinaweka uhakika wa chakula nchini, ni vyema Watanzania wakajipanga kupitia Jukwaa la mifumo ya chakula Afrika linalotarajiwa kufanyika Dar es Salaam kuanzia Septemba 5 hadi 8, mwaka huu ili nchi iweze kulilisha Bara la Afrika kwa mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi.
“Sasa agizo langu ni kwamba Wizara zinazohusika pamoja na wadau wengine wote mjipange vizuri kulitumia Jukwaa la Mifumo ya Chakula Afrika kupata masoko mazuri ya mazao yetu ya kilimo, mifugo na uvuvi ili kuboresha maisha ya watu wetu,” alisisitiza Rais Samia.