RAIS Samia Suluhu Hassan amesema amefurahishwa na matumizi mazuri ya fedha za mfuko wa tozo zinazokusanywa na Jeshi la Polisi na kutumika katika ujenzi wa kituo cha polisi Kizimkazi Mkoa wa Kusini Unguja.
Alisema hayo wakati akizindua Kituo cha Polisi Kizimkazi kilichogharimu Sh milioni 292 ambazo ni sehemu ya fedha zinazotokana na tozo zinazokusanywa na polisi.
Rais Samia alisema amefurahishwa kuona maagizo aliyoyatoa kuhusu matumizi sahihi ya fedha za polisi yakianza kufanyiwa kazi hatua ambayo itasaidia na kuwezesha jeshi hilo kutekeleza malengo yake ya ujenzi wa vituo vya polisi pamoja na nyumba za wapiganaji.
Alitaja malengo ya baadaye ya serikali ni kuimarisha Jeshi la Polisi kwa kulipatia vitendea kazi ikiwamo majengo na makazi ya wapiganaji.
“Nimefurahishwa na utekelezaji wa maagizo yangu niliyoyatoa katika mkutano wa kazi wa polisi hivi karibuni kuhusu matumizi sahihi ya fedha zinazokusanywa na jeshi kwa ajili ya shughuli za utendaji wa kazi,” alisema.
Akizungumzia kituo cha polisi cha Kizimkazi, alisema ndoto ya wananchi ya kutaka kukamilika kwa ujenzi huo imetimia. Aliwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa polisi.
Alisema kituo hicho ni mali ya wananchi na si ya Jeshi la Polisi na njia pekee ya kufanikisha matumizi yake na malengo ni kuwepo kwa ushirikiano kati ya wananchi na polisi.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni alisema Jeshi la Polisi limejipanga kuhakikisha linatumia fedha vizuri zinazokusanywa kupitia mfuko wa tozo kwenda moja kwa moja kwa Shirika la Ujasiriamali la Polisi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya polisi.
Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Hamad Khamis Hamad alisema ujenzi wa kituo hicho umegharimu Sh milioni 292 na kati ya fedha hizo Sh milioni 26 vifaa vyake vimetolewa na watu mbalimbali ikiwemo viongozi na wafadhili wengine.
“Rais ujenzi wa kituo hiki unakwenda sambamba na maagizo uliyotupa hivi karibuni kuhakikisha vituo vya polisi havitumiki kwa ajili ya kuwabambikizia kesi wananchi,” alisema.
Awali, Rais Samia alipewa taarifa ya chaguzi mbalimbali za Chama Cha Mapinduzi ambazo zilifanyika kwa mafanikio makubwa na kuwapata viongozi wa ngazi mbalimbali.