VYAMA vya siasa, wachumi na wananchi ndani na nje ya nchi wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuanza kuchukua hatua kutokana na ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Katika taarifa iliyotolewa na Ikulu Jumapili, Rais Samia alivunja Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Reli la Tanzania (TRC) na kutengua uteuzi wa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA), John Nzulule.
Aidha, Rais Samia amemuagiza Katibu Mkuu Kiongozi kuwaelekeza makatibu wakuu wa wizara na watendaji wakuu wa taasisi za serikali wasome ripoti za CAG za mwaka wa fedha 2021/2022 zilizotolewa Aprili 6, mwaka huu na wajibu hoja hizo na kuzifanyia kazi zote.
“Watendaji wote watakaobainika kuhusika na uzembe au ubadhirifu wachukuliwe hatua za kisheria,” imeeleza sehemu ya taarifa ya Ikulu.
Wabunge
Mbunge wa Vwawa, Japhet Hasunga (CCM) amempongeza Rais Samia kwa hatua alizoanza kuchukua kuhusu ripoti ya CAG.
Hasunga alisema kipindi kilichopita kulikuwa na uzito kwa upande wa serikali kuchukua hatua jambo lililosababisha mambo kuendelea kama alivyobainisha CAG.
“Ndiyo maana Rais amechukua hatua. Kitendo cha Rais kutamka, watendaji wanatakiwa kufanya mambo mawili; kuwajibika kisiasa…anayejiona amehusika kwa namna moja au nyingine inatakiwa ajipime ajiuzulu au aombe kukaa pembeni mpaka ukaguzi utakapokuwa umekamilika na kuthibitisha kama hahusiki,” alisema Hasunga na kuongeza:
“Kila mtendaji au kiongozi ajipime uzito wa masuala yanayomhusu, afanye uamuzi ulio sawa. Asipofanya uamuzi, Rais atatumia madaraka baada ya kushauriwa na vyombo ni hatua gani achukue.”
Amesifu uwazi wa CAG na kapongeza wadau vikiwamo vyombo vya habari na vyama vya siasa kwa kuchambua ripoti hizo.
Mbunge wa Biharamulo Magharibi, Ezra Chiwelesa (CCM), alisema uwazi wa CAG umechangiwa na uwezeshwaji kifedha unaofanywa na serikali chini ya Rais Samia.
Chiwelesa alisema hatua aliyochukua Rais Samia ni fursa kwa viongozi wengine waendelee kuwajibishana.
“Kuwajibika kwa nchi za Afrika si jambo jepesi. Tunachoweza kusema kila mmoja ajitafakari hata akisema amejikausha, moto kutoka kwa Rais, bunge utawababua,” alisema.
Wachambuzi wa uchumi
Mchambuzi wa uchumi, Goodluck Ng’ingo amesema uamuzi wa Rais Samia kuivunja Bodi ya Wakurugenzi TRC na kutengua uteuzi wa Mtendaji Mkuu wa TGFA ni onyo kwa watumishi wa umma.
Ng’ingo alisema Rais Samia ametuma ujumbe kwa watumishi wa umma kuwa ukitumia vibaya madaraka utawajibishwa.
Pia alisema Rais Samia ametuma ujumbe kwa watendaji wachukue hatua kwa watu wengine waliohusika katika kuisababishia hasara serikali kwa kuwa yeye ameshaonesha mfano.
“Rais ndiye mwenye mamlaka ya kuvunja bodi, lakini nafasi nyingine za utendaji za chini Waziri anaweza kufanya uwajibishaji. Kwa tafsiri kwamba amevunja bodi maana yake wengine pia wanapaswa kuchukua hatua za kinidhamu zinazostahiki kwa watendaji wa ngazi za chini ambao wako ndani ya mamlaka yao,” alisema Ng’ingo.
Mchambuzi mwingine wa masuala ya uchumi, Abbas Mwalimu alisema hatua alizochukua Rais Samia zitaleta tija endapo hatua zaidi zitachukuliwa ikiwemo kuwawajibisha wote wanaothibitika kuisababishia hasara serikali.
Mwalimu alisema endapo watu hao watawajibishwa kwa kufikishwa kwenye vyombo vya sheria na sheria kuchukua mkondo wake itasaidia kuleta tija kwenye utendaji serikalini kwa wengine wataogopa kuchezea fedha za umma.
Alisema anaona kuwa kwenye sheria kuna changamoto kwa kuwa watu wanaona kuwa wanaweza kuiba fedha za umma na maisha yakaendelea bila tatizo.
Mwalimu alisema mtu anaweza kuitia serikali hasara ya Sh bilioni 60 lakini akapigwa faini Sh milioni 12 au kifungo cha miaka mitano adhabu ambazo mtu hawezi kushindwa kuzimudu.
“Wakati huu ambapo serikali imeunda kikosi kazi cha kupitia haki jinai, kuna haja pia ya kuangalia makosa kama haya ili yaendane na kosa ambalo mtu amelifanya. Kwa mfano kama mtu ameingiza hasara hiyo, afilisiwe mali zake kama ni majumba na magari ili fedha hizo zirudi serikalini, watakapofilisiwa itajenga nidhamu na kuwajibika,” alisema Mwalimu.
Mwalimu alisema makatibu wakuu nao wanapaswa kuwawajibisha watu wengine waliobaki wanaohusishwa na hasara hiyo, lakini pia Bunge kupitia kamati zake zinazohusika linaweza kuchukua hatua.
Aidha, wachambuzi hao walisema Rais Samia amefanya vizuri kumpa uhuru CAG afanye kazi zake kwa kuwa itaimarisha utawala bora, itaongeza uwazi na wajibu wa wananchi kuishauri na kuisimamia serikali kupitia Bunge, kujenga taasisi imara inayoweza kufanya kazi bila kuingiliwa.
Pia walisema hatua hiyo inaruhusu ukosoaji ili kuboresha ufanisi katika utendaji kazi serikalini kama ilivyo kwa timu ya mpira ambayo lazima ikosolewe ili ifanye vizuri.
Wananchi
Fundi ujenzi wa Dar es Salaam, Shomari Msabaha amemhimiza Rais Samia asirudi nyuma katika mapambano dhidi ya ufisadi.
“Sisi wananchi wa Dar es Salaam tunaunga mkono juhudi za Rais Samia kupambana na ufisadi na tunamtaka asonge mbele, tuko naye bega kwa bega kwenye vita hii,” alisema Msabaha.
Mama lishe katika Mkoa wa Mwanza, Asha Bakari alimwomba Rais Samia awadhibiti maofisa wa manispaa na halmashauri za miji na wilaya ambao wanafanya ubadhirifu kwenye fedha za kuwakopesha vikundi vya kina mama.
“Serikali kila mwaka inatoa pesa kwa ajili ya kutukopesha sisi kina mama wa hali ya chini kupitia vikundi vyetu, lakini pesa hizi zimekuwa zinaliwa na maafisa wa umma wasio waaminifu na hazifiki kwetu. Tunamwomba Rais Samia akomeshe huu ubadhirifu,” alisema Asha.
Wananchi kadhaa wa Uganda na Kenya wakitoa maoni yao kupitia mitandao ya kijamii wameweka bayana shauku ya kuwa na Rais anayechukua hatua kwa haraka kudhibiti ufisadi kama Rais Samia.
ACT-Wazalendo
Chama cha ACT-Wazalendo kimependekeza Bunge liunde Kamati teule ya Bunge kuchunguza hoja tatu za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuhusu ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) likiwemo ongezeko la gharama za ujenzi.
Kiongozi wa chama hicho, Kabwe Zitto amesema hoja hizo ni nzito hivyo si busara zikasubiri utaratibu wa kawaida wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kwa kuwa mchakato huo ni mrefu.
Zitto alisema PAC itaanza kuzifanyia kazi hoja za CAG Agosti mwaka huu na itatoa taarifa mwakani hivyo wamemwomba Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson aunde kamati teule kushughulikia hoja hizo.
Alidai CAG amebainisha kuwa Benki ya Standard Chartered ndiyo iliyoamua na kuilazimisha serikali nani awe mkandarasi wa reli hiyo katika loti ya tatu na nne hivyo kusabababisha ongezeko la gharama za ujenzi.
“Kamati teule ya bunge iwaite na iwahoji Standard Chartered Bank kuhusu hili,” alisema Zitto na akasema pia kamati hiyo ihoji sababu za ununuzi wa treni kuongezeka na ipendekeze hatua za kuchukua.
Wanasiasa, wachambuzi siasa
Katibu Mkuu wa Chama cha Alliance For Democratic Change (ADC), Doyo Hassan Doyo alisema hatua za Rais Samia zitaleta mabadiliko katika utendaji wa serikali.
Doyo alisema pamoja na hatua hizo bado zinahitajika kuchukuliwa hatua za kisheria dhidi ya waliotajwa katika ripoti hiyo ya CAG.
Kuhusu uamuzi wa Rais Samia kutoa uhuru kwa CAG afanye ukaguzi na kutoa taarifa kwa uwazi kwa wananchi, alisema inaonesha kuwa anataka serikali iwe wazi zaidi katika uendeshaji wake.
“Lakini pia twende mbali zaidi vyombo vya habari viwe wazi kuandika hizi habari ili watu wazione na hatua zichukuliwe baada ya haya mambo kuibuliwa,” alisema.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Iringa (UoI) na mchambuzi wa masuala ya siasa, Samson Mwigamba alisema hatua alizoanza kuchukua Rais zinatia moyo kwa wananchi kwamba sasa ripoti za CAG zinaanza kuchukuliwa.
Mwigamba alimshauri Rais Samia achukue hatua haraka kwa wahusika ili kupunguza au kumaliza ufisadi katika serikali.
Kuhusu kipengele alichoagiza watendaji wajibu hoja, Mwigamba alisema hoja zikijibiwa vizuri zile zilizobaki alimwomba Rais Samia achukue hatua zaidi kwa wahusika ili kuondokana na zigo hilo.
“Mimi ni mhasibu kitaaluma najua kwamba hoja za CAG zinayo nafasi ya kujibiwa lakini ikitokea kuna hoja haijapata jibu sawasawa huwa inabaki zile zilizojibiwa vizuri huondolewa. Sasa zile zilizobaki Rais achukue hatua thabiti. Nilifurahi sana alivyoongea kwa ukali na kuonesha wazi kuwa sio mpole wa kuachia watu wafanye wanavyotaka. Nampongeza kwa hilo,” alisema Mwigamba.
Alisema kutokana na hatua anazoanza kuchukua Rais Samia anatuma ujumbe kwamba kwenye mambo ya msingi yenye manufaa kwa nchi na si jambo la urafiki au ukaribu na mtu.
Mwigamba alisema hata katika hotuba yake ya kwanza bungeni Aprili mwaka 2021 alieleza kwamba hatakubali kuona nchi inarudi kwenye zama za ufisadi na matumizi mabaya ya fedha za serikali.
Imeandikwa na Halima Mlacha, Matern Kayera, Anna Mwikola (Dar es Salaam) na Stella Nyemenohi (Dodoma).
Comments are closed.