RAIS Samia Suluhu Hassan amehimiza Watanzania waendelee kuwa wamoja, wakiwakumbuka watu wenye uhitaji zaidi.
Alituma ujumbe huo jana kupitia ukurasa wake katika mtandao wa kijamii wa twitter akiwatakia wananchi heri ya Sikukuu ya Idd Al Adha.
“Tusherehekee siku hii njema kwa amani, umoja na upendo, tukiwakumbuka wale wote wenye uhitaji zaidi,” aliandika Rais Samia.
Aliongeza: “Tutumie siku hii pia kuendelea kumwomba Mwenyezi Mungu azipokee ibada zetu, atusamehe makosa yetu, atuongoze katika mema, kweli na haki, tuendelee kuwa wamoja na atuepushe na yote yenye nia ya kutugawa. Eid-al-Adha Mubarak.”
Wakati huohuo, akizungumza kwa niaba ya Rais Samia kwenye Baraza la Idd El-Adha kitaifa, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisisitiza Watanzania waendelee kutunza amani, umoja, mshikamano na usalama nchini.
Katika baraza hilo lililofanyika kwenye Msikiti wa Mfalme Mohamed wa Sita Kinondoni, Dar es Salaam jana, Majaliwa alisema amani iliyopo nchini inawawezesha Watanzania kufanya ibada, kutafuta riziki na kupeleka watoto shule kwa utulivu tofauti na nchi nyingine nyingi ambako amani imetoweka.
“Viongozi wa dini mna jukumu la kufundisha na kusisitiza amani, mshikamano na kila mmoja ajione ana jukumu la kufanya Tanzania iendelee kuwa kisiwa cha amani, tudumishe amani, upendo bila kujali itikadi, imani, dini, ukabila na ukanda,” alisema Majaliwa.
Aliwakumbusa waumini wa Kiislamu kuwa wanaposherehekea sikukuu hiyo, wakumbuke wajibu wao wa kuwasaidia maskini na wote wenye uhitaji kwa kuwa kutoa sadaka kwa kundi hilo ni sehemu ya ibada.
“Tunapopata fursa ya kuchinja tuwakumbuke wote wenye uhitaji wakiwemo yatima, wajane, wazee na wengine ili tupate thawabu kwa Mwenyezi Mungu. Pia tufanye ibada ya kuwarehemu marehemu wetu, tuwaombee dua ili Mwenyezi Mungu awapunguzie adhabu, utaratibu huu uwe endelevu na tuwafunze watoto kuendelea kuwaombea marehemu wetu,” alisema Majaliwa.
Kuhusu ushirikiano kati ya madhehebu ya dini na serikali, alisema serikali inathamini uhusiano mzuri uliopo baina yake na madhehebu ya dini kwa maendeleo ya taifa.
Majaliwa alisema serikali inatambua na kuona jitihada za madhehebu ya dini na taasisi nyingine. Amewataka waendelee kuiunga mkono kuwahudumia Watanzania.