RAIS Samia Suluhu Hassan ameihakikishia nchi ya Marekani kwamba Tanzania ina dhamira ya dhati kutekeleza maeneo yaliyokubaliwa kushirikiana baina ya nchi hizo.
Amesema wakati wa ziara ya Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris baadhi ya hati za ushirikiano zimesainiwa ikiwemo hati ya ushirikiano katika bandari, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) na biashara.
Akizungumza na waandishi wa habari Ikulu, Dar es Salaam jana mara baada ya kuzungumza na Makamu wa Rais wa Marekani, Rais Samia alisema kwa niaba ya Watanzania wote, makubaliano hayo yatatekelezwa na kuheshimiwa.
Aidha, alisema ana imani ziara hiyo itakuwa ni fursa na jukwaa la kutafuta maeneo mapya ya kuwekeza.
Rais Samia alikaribisha ushirikiano na Marekani katika maeneo ya uvuvi hasa katika bahari kuu, uvuvi wa samaki, uchimbaji wa chumvi, utafiti wa mafuta na gesi, utalii na usafirishaji wa baharini.
Pia alizungumzia suala la viza na kueleza kuwa Tanzania inakaribisha utayari wa Marekani kufanya mapitio ya mkataba wa viza ya sasa ili kuwezesha raia wa nchi hizo mbili kunufaika na viza ya muda mrefu.
Rais Samia alisema Tanzania imeendelea kunufaika na misaada mbalimbali ya watu wa Marekani kama vile Mpango Unaozipa Fursa Nchi za Afrika Kuuza Bidhaa Katika Soko la Marekani Bila ya Kutozwa Kodi (AGOA).
Aliomba kurejewa kwa mkataba wa AGOA kwa sababu umekaribia kufikia mwisho kutokana na kwamba ni muhimu katika kusaidia biashara kukua.
“Kwa hiyo tunaomba kuongezewa kwa muda wa mkataba huo unaomalizika mwaka 2025 angalau uongezeke hadi mwaka 2030,” alisema Rais Samia.
Alisema nchi za Afrika ikiwemo Tanzania zinaomba kurefushwa kwa mkataba huo angalau kwa miaka 10 wawekezaji wanaowekeza nchini wanaotumia mpango huo wapate uhakika wa biashara yao kuwa endelevu.
Kuhusu demokrasia, alisema ni jambo muhimu katika serikali yake na amejitahidi kuhakikisha utawala wa sheria unazingatiwa.
“Na katika muktadha huu namshukuru Rais Joe Biden katika mkutano wa demokrasia wa mwaka 2022 niliohudhuria kwa njia ya mtandao. Mwaliko huu unatuma ujumbe kwamba juhudi zetu zinatambulika katika kujenga Taifa la demokrasia,” alisema Rais Samia.
Alisisitiza kuwa ziara hiyo ya Kamala nchini inathibitisha uwepo wa uhusiano baina ya nchi hizo mbili na kwamba ziara za viongozi wa nchi hizo zimeendelea kuimarisha uhusiano huo.
“Na ziara yako imewafanya Watanzania sasa kusubiri ziara ya Rais wa Marekani, Joe Biden na tafadhali naomba nipelekee salamu kwamba Tanzania inamsubiri,” alisema Rais Samia.
Awali, alisema kwa zaidi ya miongo sita, Tanzania imenufaika na misaada kutoka Marekani iliyogusa sekta kama vile afya, elimu, maji, usafi wa mazingira, kilimo, usalama wa chakula, maliasili, miundombinu, demokrasia, haki za binadamu na utawala bora.
Alisema katika sekta ya afya, Ukimwi na kifua kikuu havitishii tena maisha ya watu ambapo maambukizi ya Ukimwi yameshuka kutoka asilimia 7.2 mwaka 2012 hadi asilimia 4.7 mwaka 2017 na kupungua zaidi mwaka 2021.
Rais Samia alisema maambukizi mapya ya kifua kikuu yamepungua kutoka watu 306 hadi 208 kwa kila watu 100,000 na wanawake wajawazito wenye virusi vya Ukimwi sasa wana uhakika wa kuzaa watoto wasio na maambukizi.
Pia, alisema kupitia msaada wa nchi hiyo, vifo vya malaria vimepungua kutoka milioni 7.7 mwaka 2015 hadi milioni 3.5 na lengo ni kuwa na jamii isiyokuwa na malaria kabisa.
Alisema katika kulifikia lengo hilo, Tanzania iko tayari kupokea mwekezaji atakayeanzisha kiwanda cha dawa za malaria nchini ili kupunguza gharama za upatikanaji wa dawa hizo.