Samia aita wawekezaji Afrika Kusini

RAIS Samia Suluhu Hassan na Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini wamekubaliana Tanzania na Afrika Kusini zikuze ushirikiano kwenye masuala mbalimbali ikiwamo biashara na uwekezaji.

Viongozi hao jijini Pretoria jana walishuhudia kusainiwa kwa mikataba miwili ya makubaliano ya awali. Rais Samia alikwenda Afrika Kusini kwa ziara rasmi ya kiserikali.

Rais Samia alisema yeye na mwenyeji wake wamekubaliana mambo mawili ambayo ni kuongeza ushirikiano katika masuala ya ulinzi na usalama na kukuza biashara na uwekezaji.

Alisema kati ya mwaka 2013 hadi 2022 Afrika Kusini ilisajili miradi 70 katika Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 137.4 ambazo ni sawa na Sh bilioni 321 za Tanzania.

Rais Samia alisema sekta inayoongoza kwa uwekezaji kutoka Afrika Kusini ni utalii yenye miradi yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 36.3.

Rais Samia alisema miradi hiyo 70 imetoa ajira kwa Watanzania zaidi ya 2,000 na kusema ni wakati mzuri wa kuendelea kuimarisha uhusiano kwa kuongeza wigo wa kufanya biashara na uwekezaji.

“Ni wakati mzuri wa kuendelea kuimarisha uwekezaji na biashara baina yetu, wawekezaji kutoka Afrika Kusini njooni Tanzania kuchangamkia fursa za uwekezaji katika sekta ya kilimo, mifugo, usafiri, uchimbaji madini, viwanda vya dawa, utalii na nyingine,” alisema Rais Samia.

Alitoa mfano kuwa Tanzania ina hekta zaidi ya milioni 22 zinazofaa kwa kilimo cha mpunga na akahimiza wawekezaji kutoka Afrika Kusini wachangamkie fursa hiyo katika sekta ya kilimo ili kupata bidhaa hiyo karibu badala ya kuagiza mataifa ya mbali.

Rais Samia alisema uhusiano wa Tanzania na Afrika Kusini mzuri na unaendelea kuimarika kwa sababu mataifa hayo mawili ni ndugu wa muda mrefu.

“Wananchi wa Tanzania wana kumbukumbu nzuri ya uhusiano baina ya mataifa haya mawili tangu enzi za harakati wa ukombozi wa waasisi wetu Mwalimu Julius Nyerere na Nelson Mandela na utaendelea kudumu,” alisema.

Rais Ramaphosa alisema Afrika Kusini kamwe haiwezi kuisahau Tanzania kwa jinsi ilivyokuwa mstari wa mbele kusaidia ukombozi kutoka kwa utawala wa kibaguzi.

“Tanzania ilikuwa mstari wa mbele kutusaidia katika kipindi cha ukombozi iliwapa malazi, mavazi, kuwafariji na kuwalinda wapigania uhuru wa nchi yetu, katika kipindi kibaya cha ubaguzi na ukandamizwaji wa haki za binadamu. Tanzania ilitukimbilia na kutusaidia kupigania uhuru wetu,” alisema.

Rais Ramaphosa alisema uhusiano wa Tanzania na nchi hiyo umeendelea kuwa wa kirafiki na kindugu uliojenga misingi imara.

Alisema hivi sasa kampuni 250 zimewekeza nchini Tanzania na kuwa uwekezaji unaendelea kuongezeka na matumaini yao kusainiwa kwa mikataba hiyo kutaendelea kufungua fursa nyingine na kuongeza biashara zaidi kwa manufaa ya pande zote.

Habari Zifananazo

Back to top button