Samia amaliza changamoto 15 za Muungano

Rais Samia Suluhu Hassan

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Dk Selemani Jafo amesema Serikali ya Awamu ya Sita imemaliza changamoto 15 za Muungano ndani ya miaka miwili hivyo sasa zimebaki nne tu.

Dk Jafo akasema, awali kulikuwa na hoja 25 za Muungano, mbili zilipatiwa ufumbuzi mwaka 2010 na tano zilimalizwa mwaka 2020.

“Kwa hiyo tukabakiwa na changamoto 18 lakini unaona utashi wa viongozi wetu na nia katika kuimarisha Muungano ndani ya miaka miwili ya Mama Samia, awamu ya kwanza mwaka 2021 tuliweza kutatua changamoto 11 za Muungano, na hivi juzi tulitatua changamoto nyingine nne za Muungano,” alisema wakati akizungumza kuhusu miaka 59 ya Muungano.

Advertisement

Dk Jafo alisema zimebaki changamoto tatu lakini kwa kuwa moja kati ya hizo imegawanyika katika maeneo mawili zinahesabika kuwa zimebaki nne.

Awali aliwaeleza wabunge kuwa Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar umeendelea kuwa imara tangu ulipoanzishwa Aprili 26, 1964.

Dk Jafo alisema hayo bungeni Dodoma wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2023/24.

Alisema serikali inatambua kuwa Muungano ni Tunu ya Taifa na utambulisho wa Tanzania duniani hivyo ni jukumu la kila Mtanzania kuulinda, kuudumisha na kuuenzi kwa kuwa ni jambo la kujivunia.

Dk Jafo alitaja hoja nne za Muungano zilizopatiwa ufumbuzi ni pamoja na malalamiko ya wafanyabiashara wa Zanzibar kutozwa kodi mara mbili ikiwamo kodi ya mapato (PAYE) na kodi ya zuio.

“Malalamiko ya wafanyabiashara wa Zanzibar kutozwa kodi mara mbili ilitokana na kuwepo kwa utofauti wa ukadiriaji wa viwango vya thamani za bidhaa na kodi ya forodha baina ya Tanzania Bara na Zanzibar inayosababisha wafanyabiashara wa Zanzibar kulipa kodi ya ziada kwa bidhaa zinazotoka Zanzibar kwenda katika soko la Tanzania Bara,” alisema.

Dk Jafo alitaja hoja nyingine iliyomalizwa ni mkataba wa mkopo wa fedha za mradi wa ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Abeid Amani Karume (Terminal III) na ongezeko la gharama za umeme kutoka Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kwenda Shirika la Umeme la Zanzibar (ZECO).

Pia alisema hoja nne zinazoendelea kutafutiwa ufumbuzi ni mgawanyo wa mapato yatokanayo na hisa za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) zilizokuwa katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki na faida ya Benki Kuu, mapendekezo ya Tume ya pamoja ya fedha, usajili wa vyombo vya moto na uingizaji wa sukari inayozalishwa Zanzibar katika soko la Tanzania Bara.