Samia ampongeza Rais wa China

RAIS Samia Suluhu Hassan amempongeza Rais wa China, Xi Jinping kwa kuchaguliwa tena kuendelea kuwa Katibu Mkuu wa Kamati Kuu (CC) ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC).

Xi aliingia madarakani mwaka 2012 hivyo ataiongoza China kwa miaka mitano mingine kwa kipindi cha tatu.

Katika ukurasa wake katika mtandao wa kijamii wa twitter, Rais Samia jana aliandika: “Pongezi za dhati kwa Mheshimiwa Rais wa China Xi Jinping, kwa kuchaguliwa tena kuendelea kuwa Katibu Mkuu wa Kamati Kuu (CC) ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC).”

Advertisement

Oktoba Mosi, mwaka huu, Balozi wa China nchini, Chen Mingjian alisema Rais Xi na Rais Samia Suluhu Hassan wanathamini uhusiano wa China na Tanzania.

Balozi Chen alisema hayo wakati wa Kumbukumbu ya Miaka 73 ya kuanzishwa kwa Jamhuri ya Watu wa China (PRC).

Alisema China iko tayari kuunga mkono juhudi za Tanzania za kupata maendeleo endelevu sanjari na kuimarisha na kuendeleza ushirikiano baina ya nchi hizo.

Balozi Chen alisema katika nusu ya kwanza ya mwaka huu, kiwango cha biashara kati ya China na Tanzania kilifikia dola za Marekani bilioni 3.558.

“Idadi kubwa ya miradi ya ushirikiano kati ya China na Tanzania, kama vile Kituo cha Kufua Umeme wa Maji cha Julius Nyerere na Kituo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi cha Mkoa wa Kagera, inaendelea kwa kasi,” alisema Balozi Chen. Kituo hicho tayari kimezinduliwa rasmi.

Aliongeza: “Aidha, China imetekeleza kikamilifu ahadi yake ya kuisaidia Tanzania katika mapambano dhidi ya Covid-19. Hadi sasa, China imetoa dozi milioni 5.61 za chanjo ya Covid-19 kwa Tanzania.”

Desemba 7, mwaka jana Balozi Chen aliwaeleza waandishi wa habari kuwa Rais Samia alipozungumza na Rais Xi kwa simu Juni mwaka jana, walikubaliana Tanzania na China zikuze ushirikiano katika uchumi, utamaduni na ushirikiano wa kimataifa.

Alisema China iliahidi kufungua zaidi soko lake kwa bidhaa za Tanzania na kuongeza uwekezaji hususani katika sekta ya viwanda.

Balozi Chen alisifu ushiriki wa Tanzania kwenye Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) na akasema nchi hizo mbili zimekubaliana kuimarisha ushirikiano wao katika nyanja za miundombinu, afya, biashara, uwekezaji na mambo mengine mbalimbali.

 

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *