Samia ampongeza Ruto kwa kuthibitishwa

Dk William Ruto

RAIS Samia Suluhu Hassan amempongeza Rais Mteule wa Kenya kupitia muungano wa Kenya Kwanza, Dk William Ruto kwa kuthibitishwa na Mahakama Kuu ya nchi hiyo kuwa rais wa tano wa nchi hiyo. Kupitia ukurasa wake katika mtandao wa kijamii wa twitter, Rais Samia alisema anatarajia kufanya kazi na Dk Ruto kuimarisha uhusiano wa kihistoria baina ya Tanzania na Kenya.

Agosti 16 mwaka huu, Rais Samia aliwapongeza wananchi wa Kenya kwa kushiriki Uchaguzi Mkuu kwa amani na utulivu na Dk Ruto akatangazwa Rais mteule wa Kenya.

“Tanzania itaendeleza undugu na ushirikiano wa kihistoria na Kenya uliodumu miaka na miaka,” alieleza Rais Samia kupitia ukurasa wake wa twitter.

Advertisement

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Wafula Chebukati alisema Dk Ruto alishinda kwa kupata kura 7,176,142, mpinzani wake mkuu, Raila Odinga alishika nafasi ya pili kwa kupata kura 6,942,930, Waihika David Maore alipata kura 31,907 na Profesa Wajackoyah George akipata kura 61,969.

Wadau wa siasa wakiwemo viongozi wa vyama vya upinzani jana walitaja mambo kadhaa ya kujifunza kwa nchi za Afrika Mashariki katika mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa Kenya hasa amani na utulivu.

Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF), Magdalena Sakaya alisema kuna mambo mengi kwa nchi za EAC kujifunza kuhusu uchaguzi wa Kenya hasa kutanguliza maslahi ya nchi.

Sakaya alisema katika uchaguzi huo, Wakenya waliamua kuliweka Taifa lao mbele kuliko vyama vyao na ndiyo maana walikubaliana na matokeo ya IEBC na hu- kumu ya mahakama.

Aliyekuwa mgombea urais wa Chama cha Demokrasia Makini, Cecilia Mmanga, alisema uchaguzi wa Kenya unatoa mafunzo EAC ukiwemo umuhimu wa kuwa na tume huru ya uchaguzi, umuhimu wa kutunza amani na watu kuwa na hofu ya Mungu.

Mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Bubelwa Kaiza alisema kuna haja kwa nchi nyingine za EAC kuangalia katiba na tume za uchaguzi ili mtu asiporidhika apate nafasi ya kwenda mahakamani.

Katibu Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Ado Shaibu alisema nchi za Afrika Mashariki zinaweza kujifunza kupitia uchaguzi wa Kenya umuhimu wa kuwa na katiba nzuri na vyombo vinavyoundwa na katiba hiyo hasa tume huru na mahakama.