Samia ampongeza Tshisekedi, aahidi ushirikiano

MTANDAO: RAIS Samia Suluhu Hassan amempongeza Rais Mteule wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Félix Tshisekedi kwa kutetea kiti cha Urais kwa awamu ya pili.

Kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii, Rais Samia amesema matarajio yake ni kuendeleza ushirikiano wa kihistoria uliopo katika nchi hizo zenye ukwasi wa rasilimali.

“Natarajia kuendelea kufanya kazi pamoja katika kukuza uhusiano kati ya nchi zetu mbili na @Jumuiya ya Afrika Mashariki.” Ameandika Rais Samia.

Kwa mujibu wa matokeo ya Tume huru ya Uchaguzi ya nchini humo, (CENI) Felix Tshisekedi ni kinara wa uchaguzi wa Desemba 20, 2023 kwa zaidi ya asilimia 70 ya kura, huku akifuatiwa na mfanyabiashara, Moise Katumbi aliyejizolea asilimia 18 ya kura.

Mtendaji mkuu wa zamani wa kampuni ya mafuta, Martin Fayulu alipata asilimia 5, huku mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel Denis Mukwege, daktari maarufu kwa kutibu wanawake waliotendewa ukatili wa kijinsia mashariki mwa DR Congo, alipata chini ya asilimia 1.

Habari Zifananazo

Back to top button