Samia ampongeza Waziri Mkuu mpya Uingereza

RAIS Samia Suluhu Hassan amempongeza Liz Truss kwa kuchaguliwa kuwa kiongozi wa chama cha Conservative na Waziri Mkuu wa Uingereza.
Alitoa pongezi hizo jana kupitia ukurasa wake katika mtandao wa kijamii wa Twitter.
Samia alisema Tanzania inatarajia kuendeleza urafiki wake wa muda mrefu na Uingereza katika kukuza uhusiano uliopo wa kiuchumi na kidiplomasia.
Baada ya kukabidhiwa rasmi madaraka, Truss aliunda baraza lake la mawaziri na jana alikuwa na kikao cha kwanza na Baraza la Mawaziri.
Katika uchaguzi uliopita wa Chama cha Conservative, Truss alimshinda mpinzani wake Rishi Sunak kwa kupata kura 81,326 dhidi ya kura 60,399 za Sunak katika kinyang’anyiro cha uongozi wa chama hicho.
Waziri Mkuu huyo mpya mwenye umri wa miaka 47, alipata asilimia 57 ya kura zote halali zilizopigwa na kumrithi Boris Johnson ambaye alijiuzulu Julai kutokana na kukumbwa na kashifa kadhaa.
Katika hotuba yake fupi baada ya ushindi, Truss aliahidi kuja na mipango madhubuti ikiwemo ya kupunguza kodi, kujenga uchumi na kushughulikia matatizo yanayohusu suala la nishati kwa ujumla wake.
Truss alizaliwa katika mji wa Oxford na nyumbani kwake ni London na Norfolk, pia ni mbunge wa Jimbo la Norfolk Kusini Magharibi.