Samia:  Anayepewa dhamana asiwe mzembe

Rais Samia

RAIS  Samia Suluhu Hassan amesema kumekuwa na malalamiko, manung’uniko na kelele kutoka kwa wazazi na ndugu wa vijana wanaoondolewa kazini kwenye ofisi za umma na kutaka waache kelele hizo.

Amesema kila mtu ana haki sawa, anayeonekana anafaa ndie atawekwa kwenye nafasi na wao kama viongozi huwa na macho marefu ya kugundua nani anafanya vizuri na nani hafanyi vizuri.

Advertisement

Rais Samia ameyasema hayo leo Julai 16, 2023 katika Kongamano la Wanawake wa Kiislam Zanzibar katika maadhimisho ya Mwaka Mpya wa Kiislamu 1445 – Hijiria.

Amesema, anayepewa dhamana asiwe na mkono, asiwe mzembe akaacha kazi akaenda vijiweni.

“Tuna mambo mengi tumetoa haki za ndani na nje, lakini unaona kabisa fulani nikimtoa hapa nikamuweka fulani pataenda vizuri tuache kelele tuwapeni viongozi wetu fursa ya kufanya kazi.

“Tustahimili mdogo wako kuondoka, mwanao kuondoka tunyooshane toka nyumbani, mtu tukiona hafai tutamtoa.

“Kila anaishi Zanzibar ana haki ya kufanya kazi na kupata fursa, manung’uniko ya nini tuacheni kelele,” amesisitiza na kuongeza.

“Kumekuwa na maneno mengi sana kawekwa huyo, kachukua watu wa huko tu, kafika tu kawaondosha watu wote sijui kafanyaje? Udhalilishaji hudumaza maendeleo.

“Mungu kanipa mtihani si haba, pale aliponiweka, na ukisikiliza ya watu Samia Suluhu yule mmm…mtihani si haba nilio nao, nijiusie nafsi yangu kwanza, na niwausie na wengine,  wote tushiriki na wote tuige mifano mizuri tunayooneshwa na viongozi wa dini hasa kutumia njia bora na hekima katika kuendesha maisha yetu.

“Tulioshika madaraka tuwe thabiti, tuwe na hekima katika kutoa maamuzi, sio unapewa dhamana husikilizi wengine, mtu anakuja na shida zake fulani msikilize huyo, kuweni wastarabu, sio kuweka mabega juu kama mizani ukipewa madaraka wanaume koti zinaninginia, wanawake shungi zipo sivyo,” amesema.

 

4 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *