Samia anogesha ujenzi vyuo vya Veta

TABORA: VYUO 64 vya Ufundi Stadi (VETA) vitajengwa nchi nzima, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mipango ya serikali kujenga vyuo hivyo kila wilaya nchini.

Hayo yamesemwa leo Oktoba 17, 2023 na Rais Samia Suluhu Hassan katika hafla ya kuweka jiwe la msingi katika chuo cha VETA wilayani Igunga, ikiwa ni ziara yake ya kikazi Mkoa wa Tabora.

“Chuo hiki ni sehemu ya jitihada ya serikali kuwapa vijana elimu ya amali, ili waweze kujiajiri au kuajiriwa,” amesema Rais Samia.

Rais Samia amesema mikakati ya serikali ni kuhakikisha kila mkoa nchini kunakuwa na chuo cha VETA cha Mkoa, lengo ni kuwawezesha wananchi kuwa na ujuzi wa kutumia fursa zilizopo katika maeneo yao.

Rais amewataka wananchi wa Tabora kulima kwa juhudi, kwani masoko ya mazao yao ni ya uhakika na kwamba serikali inaendelea na juhudi za kuwatafutia masoko nje ya nchi, na pindi masoko yanapokuwa changamoto serikali itayanunua mazao yao.

Habari Zifananazo

Back to top button