Samia apongeza benki mikopo bila riba

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema amefurahishwa na kujitokeza kwa taasisi za fedha na benki nchini kushuka chini na kuwafikia moja kwa moja wananchi kwa kuwapatia fedha za mikopo isiyokuwa na riba kwa ajili ya kuendesha biashara zao.

Akizungumza na wananchi Kizimkazi Mkoa wa Kusini Unguja katika kilele cha Tamasha la Kizimkazi alisema mikopo isiyokuwa na riba ni fursa muhimu ambayo itawawezesha wajasiriamali na wananchi kwa ujumla kunufaika na kujikomboa kiuchumi.

Aliongeza kuwa katika tamasha hilo, alipotembelea mabanda ya maonesho alivutiwa na kushuhudia taasisi za fedha  zikiwafikia moja kwa moja wananchi wakiwemo wajasiriamali wanawake na kuwapatia fursa ya kufungua akaunti hapohapo.

Alisema wananchi wengi wakiwamo wanawake sasa wamepata mwamko mkubwa na wako tayari kuchukua mikopo kwa ajili ya kuendesha biashara zao yenye masharti nafuu.

“Nimefurahishwa na kazi kubwa inayofanywa na taasisi za fedha na benki kwa kushuka chini na kuwafikia wananchi moja kwa moja na wengine kufungua akaunti,” alisema.

Rais aliitaja mikakati inayotarajiwa kuchukuliwa na Mkoa wa Kusini kwa ujumla ni kufikisha huduma za elimu ikiwamo kuongeza ufaulu wa wanafunzi katika mitihani ya taifa.

Kwa mfano alisema kiwango cha ufaulu wa elimu katika Mkoa wa Kusini Unguja si ya kuridhisha ambapo kupitia taasisi ya Mwanamke Initiative Foundation (MIF) itahakikisha inafanya kazi kubwa ya kuhamasisha vijana wakiwemo mtoto wa kike kupiga hatua kubwa ya maendeleo katika elimu.

Samia alisema atahakikisha kazi ya ujenzi wa shule unaongezeka na kufurahishwa na ufunguzi wa ukumbi wa mikutano katika shule ya Kizimkazi ambao utatumiwa na wanafunzi kwa ajili ya kufanya mitihani ya majaribio pamoja na ufunguzi wa maabara ya sayansi.

Kuhusu sensa ya watu na makazi, Rais Samia aliwapongeza wananchi nchini kote kwa kujitokeza kwa wingi na kuifanikisha.

Alisema sensa imekuwa ya mafanikio makubwa kutokana na ushirikiano na wananchi walivyohamasika kuhesabiwa hatua ambayo kwa kiasi kikubwa imefanikisha malengo ambayo ni kujua idadi ya watu na shughuli zao za kiuchumi na maendeleo.

“Nachukua nafasi hii kuwapongeza wananchi wa Tanzania kwa kukubali kuhesabiwa hatua ambayo itafanikisha malengo ya serikali kujua idadi ya watu wake..tumeongeza siku saba tutafanya sensa ya kufahamu nyumba na makazi,” alisema.

Mapema Rais Samia aliwatahadharisha Watanzania na kusema ugonjwa wa Covid-19 bado upo na tishio kwa afya ya binadamu na kuwataka wananchi wasijiachie bali waishi kwa kuchukua tahadhari zote muhimu ikiwemo kupata chanjo.

“Nilipoingia katika uwanja huu mimi na ujumbe wangu ndiyo pekee tuliojikuta tumevaa barakoa na sisi tukazivua…kuacha kuvaa barakoa maana yake watu wamechoka nazo,” alisema.

Aidha, aliitaka Wizara ya Afya kuja na mwongozo na kutoa taarifa rasmi kuhusu suala la barakoa kama wananchi waendelee kuvaa au kuziacha wakati ugonjwa huo ukiwa bado upo.

Akimkaribisha Rais, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliwataka Watanzania kumuunga mkono Rais Samia na katika kipindi kifupi amefanya kazi kubwa ya kuwaunganisha wananchi wa Tanzania na kufungua milango ya uwekezaji kiuchumi.

Alisema ubunifu wake katika filamu ya Royal Tour umefungua milango katika sekta ya utalii na kwa upande wa wananchi wa Kizimkazi ni mfano wa kuigwa kwa kutembelewa na idadi kubwa ya watalii wanaokuja kuangalia vivutio.

Alisema Tanzania inashuhudia idadi kubwa ya watalii katika maeneo yote ikiwamo Serengeti na Ngorongoro hatua ambayo ni matunda ya kazi kubwa iliyofanywa na Rais Samia na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi.

Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Rashid Hadid Rashid akitoa taarifa ya tamasha hilo la Kizimkazi alisema limepiga hatua kubwa na kuitangaza Zanzibar katika sekta ya utalii.

Alisema Mkoa wa Kusini pamoja na Kijiji cha Kizimkazi kwa ujumla wake kimepokea idadi kubwa ya watalii 47,000 mwaka 2020 huku idadi ikiongezeka siku hadi siku kutokana na kuwapo kwa vivutio vizuri na ukarimu wa wananchi wa kijiji hicho.

Alisema tamasha hilo limekuwa chachu ya kufungua miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya na kuwawezesha wananchi kwa njia ya kuzisaidia na kujenga uwezo saccos.

Habari Zifananazo

Back to top button