RAIS Samia Suluhu Hassan amewapongeza waandishi wa habari kwa kazi nzuri ya kujenga nchi.
Alitoa pongezi hizo jana alipozungumza nao kwa njia ya simu kupitia kwa Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa.
Msigwa alizungumza na waandishi wa habari wa Mwanza kuwapa taarifa kuhusu utendaji wa serikali.
Rais Samia aliwaeleza kuwa Tanzania ni nchi ya wote na itajengwa na watu wa kada zote.
“Waandishi habari za kazi, hongereni kwa kazi Msigwa aliniambia atakuwa huko nanyi hivyo msiache kumuuliza chochote akishindwa kujibu basi mimi nitajibu mwenyewe nitakapokuja huko au hata Waziri Mkuu atakapotembelea atajibu maswali yenu,” alisema na kuongeza;
“Mnafanya kazi nzuri hivyo nawasihi muendelee hivyo kwani Tanzania ni nchi yetu itajengwa na Rais, Makamu na wananchi wote kutoka katika kada zote na baada ya hapo muwajulishe wananchi mtakayoambiwa.”
Msigwa aliwaeleza waandishi wa habari kuwa muswada wa marekebisho ya Sheria ya Huduma za Habari Namba 12 uliwasilishwa bungeni juzi na kwamba watakwenda kujadiliana na wadau juu ya waliyokubaliana kuyarekebisha.
Alisema licha ya waandishi wa habari kuwa na uhuru wanatakiwa kuzingatia sheria kwa kuwa uhuru una mipaka na hakuna mtu aliye juu ya sheria.
“Tufanye kazi huku tukizingatia sheria kwa sababu muswada huu umezingatia maoni ya wadau hivyo tufanye kazi kwa kuzingatia sheria zote. Serikali imechukua hatua ya kuangalia masuala ya uchumi wa vyombo vya habari naahidi tutakusanya maoni na mapendekezo yote ili kujua sababu za kuyumba kwa uchumi wa vyombo vyetu,” alieleza Msigwa.