WACHAMBUZI wa masuala ya uchumi wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuiongoza vizuri nchi kukiwa na changamoto likiwamo janga la Covid-19 na kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi.
Hivi karibuni, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba aliwaeleza wabunge kuwa kati Januari hadi Septemba 2022, uchumi ulikua kwa wastani wa asilimia 5.2 ikilinganishwa na asilimia 4.8 katika kipindi kama hicho mwaka 2021.
Dk Mwigulu alisema hayo Dodoma wakati akiwasilisha Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2023/2024.
Dk Mwigulu alisema ukuaji chanya wa uchumi ulichangiwa na jitihada zinazoendelea kuchukuliwa na serikali ikiwamo mikakati ya kukabili athari za vita kati ya Ukraine na Urusi na uwekezaji wa kimkakati katika miundombinu ya nishati, maji, afya, elimu, barabara, reli na viwanja vya ndege.
Alitaja sababu nyingine ni kuongezeka kwa uzalishaji wa madini hasa dhahabu na makaa ya mawe na kuongezeka kwa mikopo katika sekta binafsi ambayo imechochea shughuli za kiuchumi.
“Aidha, ukuaji huu ulichangiwa na kuongezeka kwa shughuli za utalii kutokana na kampeni ya Royal Tour. Ukuaji huu wa uchumi unaashiria kuimarika kwa shughuli za kiuchumi katika sekta mbalimbali pamoja na kuongezeka kwa ajira na mapato ya ndani,” alisema Dk Mwigulu.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti Kuondoa Umasikini (Repoa), Dk Donald Mmari alisema uchumi umeimarika kwa kuwa Rais Samia ameifungua nchi.
“Juhudi alizozifanya zimekuza mitaji ya uwekezaji, amefanikiwa kupata mikopo yenye riba nafuu kutoka Benki ya Dunia na IMF kwa ajili ya kuwekeza maeneo ambayo yaliathirika ikiwemo katika huduma za jamii na kuendeleza miradi ya miundombinu ambayo imeongeza mzunguko wa fedha kwenye uchumi kuliko miaka miwili iliyopita,” alisema Dk Mmari.
Alisema serikali imejitahidi kudhibiti mfumuko wa bei na kwamba kama nchi inahitaji fedha za kutosha kukabili mabadiliko ya tabianchi ili kuongeza uzalishaji.
Dk Mmari alieleza sekta za uzalishaji ikiwamo kilimo zinahitaji msukumo zaidi na kuongezwa fedha ili kuongeza uwekezaji na kuvutia vijana kushiriki uzalishaji wa mazao mbalimbali.
“Juhudi za kuongeza eneo la umwagiliaji litasaidia kuwa na kilimo cha maendeleo na endelevu ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, pia ni lazima kuchukua hatua za kubadilisha muundo wa kiuchumi kuhakikisha sekta ya viwanda inakua na kuongeza thamani ya mazao,” alisema.
Alisema mradi wa kilimo biashara kwa vijana utasaidia kuongeza uzalishaji hivyo uwekewe mipango ili uwe endelevu kwa kuangalia mnyororo wa thamani katika maeneo yote ya kimkakati.
Mchambuzi wa masuala ya uchumi na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Humphrey Moshi alisema Covid- 19 iliharibu mnyororo wa thamani na kusababisha uchumi kushuka kutoka asilimia 6.9 hadi asilimia nne.
“Amefanya jitihada nyingi ambazo zimechangia uchumi wa Tanzania kutodumaa kama mataifa mengine duniani. Mikopo aliyokopa na misaada aliyopata imesaidia kuimarisha uchumi wetu,” alisema Profesa Moshi.
Mkurugenzi wa Chama cha Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), Nebart Mwapwele alisema katika miaka miwili ya Rais Samia, sekta ya kilimo imepewa msukumo kwa kuongezwa bajeti na jitihada zikiendelea watafikia ukuaji wa asilimia 15 kwa mwaka ambayo itakuwa kiwango cha juu.
“Kumekuwa na mahitaji makubwa ya chakula duniani na Tanzania ina fursa ya kulisha huko. Kitendo cha kuagiza mchele au bidhaa za vyakula kutoka nje si salama kwetu kwa sababu tuna nafasi ya kuzalisha na kazi iliyopo ni kumwagilia ili wakulima wazalishe mara mbili kwa mwaka badala ya mara moja,” alisema Mwapwele.
Pia alisema bado kuna changamoto ya pembejeo na vifaa vya kilimo hivyo ruzuku endelee kutolewa na mfumo unaotumika ubadilishwe ili sekta binafsi ihusishwe kuongeza ruzuku na kusimamia uzalishaji na upatikanaji wa mbolea.
Alieleza ni lazima kuwa na viwanda vya kuchakata bidhaa hizo za kilimo, matunda na mbogamboga na kwamba katika uendeshaji wake, vinahitaji miundombinu ya umeme na barabara hivyo wanaamini mipango ya kuongeza umeme yatasaidia uzalishaji wa viwanda.
Alisema Rais Samia ameleta mabadiliko katika biashara kwa kuondoa vikwazo ikiwamo kutozuia akaunti za wafanyabiashara na kutaka majadiliano ya kodi bila kulazimisha.
Mchambuzi wa diplomasia ya uchumi, Abbas Mwalimu alisema Rais Samia ameimarisha uwekezaji na kumwezesha mwananchi mmoja mmoja kunufaika.
Alisema ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli na bandari una manufaa kwenye kiuchumi, na kwa miaka miwili uchumi umekua kwa sababu ajira zimeongezeka.