Samia apongezwa uwekezaji wa tri 37/-

Rais Samia Suluhu Hassan

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuvutia uwekezaji wenye thamani ya dola za Marekani bilioni 16 ambazo ni sawa na shilingi trilioni 37 za Tanzania katika siku 558 tangu aapishwe kuwa Rais wa Tanzania.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka alisema katika muda huo Rais Samia ametekeleza falsafa ya uchumi kuongozwa kwa misingi ya kiuchumi.

Samia aliapishwa Machi 19 mwaka jana. Aidha Shaka alisema Rais Samia ameimarisha ukusanyaji mapato na kuboresha mifumo ya kodi ikiwemo kuondoa ukusanyaji wa mabavu.

Advertisement

Alisema hayo Kibaha mkoani Pwani jana alipotembelea Maonesho ya Tatu ya Uwekezaji na Biashara mkoani humo. Shaka alitaja misingi hiyo ya kiuchumi kuwa ni pamoja na kuvutia wawekezaji, ushirikishaji sekta binafsi na kutumia diplomasia badala ya mabavu katika kufungua uchumi.

“Sote ni mashuhuda, tumeanza kushuhudia akiruhusu misingi ya falsafa za uchumi kuongoza uchumi badala ya nguvu za kiutawala. Tumeshuhudia Rais Samia akitumia taaluma yake ya uchumi na uzoefu wake wa kiuongozi na masuala ya kidiplomasia akibadili kabisa mazingira na kasi ya utekelezaji wa mipango ya maendeleo,” alisema.

Shaka alisema Rais Samia ametafuta na kuvutia wawekezaji, kuimarisha mazingira ya biashara na kuongeza shughuli za uzalishaji zitakazoongeza ajira na mapato ya serikali.

“Takwimu zinaonesha katika muda mfupi wa uongozi huu wa Rais Samia Suluhu Hassan amevutia uwekezaji wenye thamani ya dola za Marekani bilioni 16 sawa na sh trilioni 37. Huu ni ushahidi kuwa Rais Samia amedhamiria kuifanya Tanzania nguzo ya uchumi Afrika,” alisema.

Shaka alisema Rais Samia ameondoa urasimu, ukusanyaji kodi wa mabavu, kufanya maboresho ya sheria na mifumo ili kuondoa kero kwa wafanyabiashara na wawekezaji ikiwa sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020-2025, Ibara 22, 46 na 49.

“Kupitia diplomasia ya uchumi Rais amefanikiwa kutafuta wawekezaji, kuimarisha mazingira ya biashara na kuongeza shughuli za uzalishaji zitakazoongeza ajira na mapato ya serikali,” alisema Shaka.

Aliongeza: “Leo tunashuhudia wawekezaji popote walipo wanaweza kukamilisha taratibu zote za kusajili miradi na upatikanaji wa vibali vyote kutpitia kituo kimoja kwa njia ya mtandao, yaani dirisha la uwekezaji kielektroniki (Tanzania Investment Electronic Window),” Shaka alisema Rais Samia ameiongoza Tanzania kuridhia mkataba wa kujiunga na eneo huru la biashara Afrika (AFCFTA) hatua itakayoiwezesha nchi kutumia nafasi yake ya kijiografia kunufaika na soko kubwa barani Afrika lenye takribani watu bilioni 1.3 na pato ghafi la jumla ya dola za Marekani trilioni 3.4 kwa kuuza bidhaa na huduma.

“Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameonesha mwelekeo wa kuifungua nchi kiuchumi kupitia uwekezaji wa kongani za kiuchumi (Economic parks) zikihusisha kongani za viwanda (Industrial parks), kongani za teknolojia (technology parks), kongani za uongezaji thamani (Processing parks) na kongani za kilimo (Agricultural parks),” alisema.

Shaka aliwapongeza viongozi wa Mkoa wa Pwani kwa ubunifu wa kuanzisha maonesho ya uwekezaji na biashara ambayo alisema yatachochea uwekezaji na biashara.

“Ni lazima wakati wote mjipange kimkakati ili kunufaika na fursa zote za uwekezaji na biashara kwa manufaa ya uchumi wa mkoa pamoja na mwananchi mmoja mmoja,” alisema.

Akiwa katika maonesho hayo, Shaka alitembelea mabanda yakiwemo ya taasisi za umma, binafsi na wajasiriamali ambao wameyatumia kuonesha bidhaa na huduma wanazozitoa.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *