Samia aridhia Mulamula kugombea ukatibu Madola

Samia aridhia Mulamula kugombea ukatibu Madola

RAIS Samia Suluhu Hassan ameridhia Balozi Liberata Mulamula kugombea nafasi ya Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola akiamini kuwa kutokana na uzoefu wake mkubwa katika masuala ya diplomasia atakuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha uhusiano wa Tanzania na jumuiya hiyo.

Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa aliliambia HabariLEO kuwa kuchaguliwa kwa Balozi Mulamula ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Afrika Mashariki kutakuwa na manufaa makubwa kwa kuwa atasaidia baadhi ya ajenda za Tanzania kuzingatiwa ndani ya jumuiya.

“Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imepitisha jina lake na inamuunga mkono kwa sababu inaamini juu ya uwezo wake, ataiwakilisha nchi vizuri, atakuwa balozi mzuri kwa Tanzania na Afrika kwa ujumla,” alisema.

Advertisement

Msigwa aliwaomba wajumbe watakaohusika katika kumpitisha Balozi Mulamula kumpa kura za kutosha kwa sababu atatoa mchango mkubwa katika maendeleo ya jumuiya hiyo na dunia kwa ujumla.

Mbali na nafasi ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambayo aliwahi kuitumia kuanzia mwaka Machi 2021 hadi Oktoba 2022, Balozi Mulamula alikuwa Balozi wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa Mjini New York na Balozi wa Tanzania nchini Marekani na Canada.

Akiwa mwanadiplomasia wa Tanzania, Balozi Mulamula alishiriki katika Mkutano wa 77 wa Hadhara Kuu ya Umoja wa Mataifa Mjini New York, Mkutano wa 26 wa Jumuiya ya Madola uliofanyika Mjini New York na Kigali nchini Rwanda. Mwaka 2018, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres alimteua kuwa mmoja wa washauri wake wa kujenga amani na kuondoa migogoso duniani kwa kipindi cha miaka miwili.

Mbali na hayo, Balozi Mulamula alishiriki pia katika kutafuta amani katika mataifa ya Eneo la Maziwa Makuu katika nchi za Burundi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) pamoja na vikundi vya waasi katika nchi hizo. Uchaguzi wa Jumuiya ya Madola ambao Balozi Mulamula anagombea nafasi ya Katibu Mkuu unatarajiwa kufanyika mwaka 2024 huku kampeni zikianza kutimua vumbi mwaka huu.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *